Tamu, chungu ya kuhamia mfumo wa matangazo ya dijitali

Wananchi wakiwa kwenye foleni ya kununua Ving'amuzi eneo la Bamaga jijini Dar es Salaam katika siku  za mwisho kabla ya mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuhamasisha matangazo ya televisheni kutoka mfumo wa Analojia kwenda Digitali kwa Mkoa wa Dar es Salaam Desemba29 2012.Picha ya Maktaba.

Muktasari:

Maadhimisho hayo yamefanyika ikiwa ni mwaka mmoja na nusu wa mafanikio na changamoto tangu kuanza safari ya kuingia katika matangazo ya dijitali, ambayo ilianza rasmi Januari mosi, mwaka 2013 na kukamilika miezi mitatu iliyopita.

Tanzania jana imeungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha uzimaji rasmi wa mfumo wa matangazo ya analojia, huku ikiwa ni miongoni mwa nchi za kwanza katika nchi zilizo kusini ya Jangwa la Sahara.

Maadhimisho hayo yamefanyika ikiwa ni mwaka mmoja na nusu wa mafanikio na changamoto tangu kuanza safari ya kuingia katika matangazo ya dijitali, ambayo ilianza rasmi Januari mosi, mwaka 2013 na kukamilika miezi mitatu iliyopita.

Ujio wa matangazo ya dijitali umefungua fursa mbalimbali za kiteknolojia, kihuduma na kibiashara kwa watoa huduma za televisheni, wafanyabiashara wadogo wadogo, mafundi na wananchi.

Kauli ya TCRA

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma anasema kuwa Tanzania imepiga hatua kwa kuwa mpaka sasa kuna visimbuzi milioni moja sokoni.

Anasema kuwa mafanikio hayo yametokana na uamuzi wa Serikali kuweka sheria, taratibu na kanuni ambazo wadau wamezitambua, tofauti na ilivyo katika nchi nyingine za Afrika, ambazo bado hazijazima mfumo wa analojia.

Profesa Nkoma anasema kwamba mamlaka hiyo iliwashawishi watu kununua visimbuzi, lakini haikuwa na maana kuwa vyote vitakuwa na chaneli za ndani, ambazo zinaonyeshwa bure.

Anaeleza kwamba baadhi ya visimbuzi ni vya kibiashara, hivyo haiwezekani kulazimishwa kuweka chaneli za bure za kitaifa. Anavitaja visimbuzi hivyo vinavyopaswa kuonyesha chaneli tano za bure kuwa ni Digitek, Continental, Startimes na Agape.

Faida za dijitali

Matokeo ya ripoti iliyotolewa na jopo la wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ya mwaka 2013, yanabainisha faida za kutumia mfumo wa dijitali katika mawasiliano kuwa ni pamoja na kupata sauti na picha bora na matumizi bora ya masafa, ambapo chaneli moja ya analojia hutumiwa na kituo kimoja cha utangazaji wakati kwa mfumo wa dijitali chaneli hiyo hutumiwa na vituo zaidi ya kumi.

Faida nyingine ni kuwa mitambo ya kurusha matangazo kutumia nguvu ndogo ya nishati na kuwepo kwa luninga za mkononi (Mobile TV) kwenye mfumo wa dijitali.

Wananchi wanasemaje?

Wakati TCRA na baadhi ya wadau wakijivunia mafanikio ya mchakato huo yakiwemo kuongeza nafasi kubwa ya masafa na urahisi wa kurusha matangazo, bado kuna baadhi ya wananchi wanahaha kuendana na teknolojia hususan kumudu gharama za huduma husika.

Fundi wa kufunga madishi ya matangazo ya televisheni mkoani Mtwara, Ali Mnunduma anasema kuwa idadi ya wanaotumia visimbuzi imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na kupata wateja wengi wanaotafuta huduma za kufungiwa madishi hayo kwenye makazi yao.

“Ukilinganisha na mwaka jana, kwa sasa watu wameamka hasa baada ya Serikali kutangaza kuwa wanazima matangazo ya analogia Songea na Mtwara, lakini wengi bado wanalalamika kuwa hawawezi kulipia Ankara za kila mwezi, hivyo tuwashauri au tuwatafautie visimbuzi vyenye chaneli zote za ndani na vya bei nafuu,” anasema Mnunduma.

Maumivu na mkanganyiko wa uelewa juu ya kupata visimbuzi vyenye chaneli tano za taifa za bure na vyenye ahueni ya malipo, vinazidi kutesa idadi kuwa ya Watanzania na kuwafanya baadhi kununua kisimbuzi zaidi ya kimoja au kushindwa kabisa na kubaki kuangalia mikanda ya video pekee.

“Ni kweli lazima tuendane teknolojia kama Serikali inavyotaka lakini ‘bill’ (Ankara) za kila mwezi zinatuumiza sana hasa pale unapotaka chaneli nzuri, kuna baadhi ya ving’amuzi ikiisha fedha yako hupati hata TBC,” anaeleza Abdallah Khamis mkazi wa Vingunguti, jijini Dar es Salaam.

Khamis anasema kuwa amenunua visimbuzi vya aina tatu tofauti, vingine vikiwa vya madishi bila kuridhika na huduma zinazotolewa na kuamua kuvitumia wakati anapopata pesa pekee.

“Unapokuwa na biashara lazima uangalie soko likoje, biashara inaendaje na ubora wa huduma, sio kama karanga ukienda sokoni utakuta hazina thamani kwa kuwa kila mtu anazo,” anaeleza Profesa Nkoma, alipoulizwa iwapo kuna uwezekano wa kuongeza watoa huduma wengine wa visimbuzi ili kuongeza ushindani na kushusha bei ya bidhaa hizo.

Ukweli wa idadi ya Watanzania wasiopata huduma ya televisheni kutokana na kutomudu gharama za kununua visimbuzi na zile za mwisho wa mwezi, bado ni giza nene kutokana na kutokuwepo utafiti mpya zaidi zile za mwaka 2013.

Utafiti wa UDSM

Matokeo ya utafiti wa Chuko Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), yanaonyesha kuwa asilimia 89 ya kaya zilikuwa zikitumia huduma ya matangazo kwa mfumo wa kidijiti bila matatizo baada ya uzimaji wa mitambo ya analojia kwenye miji saba ilikofanyika tathmini, huku asilimia 11 ya kaya zikishindwa kupokea matangazo hayo kwa sababu mbalimbali.

Ripoti hiyo ilibainisha kwamba kati asilimia hizo 11, asilimia 5.5 hawakununua visimbizi, asilimia 0.1 walisema vilikuwa havipatikani, asilimia 3.2, walisema bei ipo juu na asilimia 0.2 walisema visimbuzi vyao vilikuwa vibovu.

“Zoezi hili halijawanyima Watanzania haki ya kupata habari kwani wengi tayari wameshajiunga na mfumo huu mpya. Jopo liliona kuwa sababu ya malalamiko mengi ni tabia halisi ya wanadamu kuogopa mabadiliko,” inasema ripoti ya UDSM.

Utafiti Twaweza

Hata hivyo, ripoti hiyo inakizanzana na ile iliyotolewa na Taasisi ya Twaweza, Novemba 2013, iliyoonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam hawakukubaliana na uamuzi wa Serikali kufunga mfumo wa analojia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo namba 21, inaonyesha kuwa gharama za kununua king’amuzi, kukilipia kila mwezi na mwonekano hafifu zilichangia uharakishaji wa watumiaji wa televisheni kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali.

Pamoja na gharama kununua visimbuzi na gharama za kila mwezi, kuna kila dalili kuwa Watanzania watahitajika tena kutoboa mifuko yao zaidi ili kuangalia televisheni kutokana na kuongezeka kwa bei ya vifaa hivyo na huduma, baada ya kasi ya kushuka kwa thamani ya Shilingi.

Kaui ya Tido

Naibu Mtendaji Mkuu wa Azam Televisheni, Tido Mhando anasema kuwa Tanzania imefanikiwa kutokana na utayari wa wadau na ari ya Serikali katika kusimamia mchakato wa kuhamia dijitali tofauti na ilivyokuwa katika nchi nyingine ikiwemo Kenya.

Tido aliyeliongoza Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) katika hatua za kuingia mfumo wa dijitali anasema changamoto kubwa zilizosalia ni uwezo mdogo wa baadhi ya wananchi kushindwa kulipia huduma za kila mwezi za visimbuzi na mkanganyiko miongoni mwao katika kupata king’amuzi kinachokidhi mahitaji yote ya huduma ambazo zinaweza kutatuliwa na baina ya Serikali na wadau.

Hata hivyo, matumaini ya kushuka zaidi bei ya huduma za visimbuzi kwa sasa ni hafifu huku Tido akibainisha kuwa gharama za uendeshaji (hasa uingizaji visimbuzi na ununuzi wa maudhui ya nje) zimeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi hali itakayozisukuma kampuni zinazohusika kuongeza bei.

“Watoa huduma (subscribers) wananunua maudhui ya nje kwa fedha za kigeni kuuza Tanzania. Kwa sababu na sarafu yetu imeshuka...kuna uwezekano mkubwa kupandisha bei ya ving’amuzi kwa sababu havina faida tena.”

“Wananchi nao lazima waelewe hivyo na suala zima la hali ya uchumi wa nchi linaathiri mambo mengi…huenda hao watu wa ving’amuzi wangetaka kushusha bei, lakini hawawezi kwa sababu hawana njia nyingine labda shilingi iimarike siku za karibuni,” anasema Tido.

Njia mbadala

Vilio vya Watanzania wasio na uwezo wa kumudu gharama hizo vinaweza vikatatuliwa iwapo Serikali itatoa ruzuku au unafuu wa kikodi kwa wasioweza kununua visimbuzi, kudhibiti bei ya malipo ya mwezi na kutumia njia mbadala zisizo za kulipia, kama anavyoeleza Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliaono, Dk Geoffrey Karokola.

“Kwa wale ambao hawawezi kulipia kila mwezi wanaweza kununua televisheni yenye king’amuzi ndani na kupata chaneli za bure zaidi ya 90 na mimi natumia hivyo,” anaeleza Dk Karokola wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Pia, kwa wenye televisheni zisizo za dijtali wanaweza kununua visimbuzi visivyo na gharama za kila mwezi kwa kufunga madishi ya mfumo wa C-Band au Ku na watapata chaneli za ndani na nje bure.”

Imeandikwa na Nuzulack Dausen, Goodluck Eliona na Emma Kallu.