Algeria wasusia uchaguzi wa Rais

Muktasari:

Waandamana na kudai kuwa uchaguzi huo ni kiini macho.

Algiers, Algeria. Wananchi wa Algeria wameandamana katika mitaa mbalimbali ya mji wa Algiers kupinga uchaguzi wa Rais kwa madai kuwa ni kiini macho.

Tume ya Uchaguzi nchini Algeria ilitangaza Alhamisi Desemba 12 kuwa ni siku ya Uchaguzi Mkuu wa rais.

Hata hivyo, muda mfupi baada upigaji kura kuanza wananchi walivamia vituo vya kupigia kura kwa madai kuwa kulikuwa na udanganyifu mwingi.

Vituo kadhaa vya kupigia kura katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo vilivamiwa na wafuasi wa vyama vya upinzani na kuzuia shughuli za upigaji kura.

Kwa mujibu wa waandamanaji hao, Tume ya uchaguzi imeshindwa kuzuia vitendo vya hila vinavyofanywa na chama tawala.

Waandamanaji hao walisema wagombea katika uchaguzi huo wapo karibu na aliyekuwa Rais wa nchi Hiyo, Abdelaziz Bouteflika.

Algeria ilikabiliwa na mgogoro wa kisiasa kwa muda wa miezi 10 sasa nuliosababisha kujiuzulu kwa Bouteflika baada ya kutawala nchi hiyo kwa mika 20.

Awali mkuu wa majeshi aliyeandaa uchaguzi huo, Ahmed Gaid Salah alisema kupatikana Rais mpya ndio njia pekee ya kuiondoa Algeria kwenye machafuko.