Alshabab wamekiri kuivamia hoteli Mogadishu iliyo karibu na ofisi ya rais

Mogadishu, Somalia. Kundi la Al-shabab limeshambulia hoteli ya kifahari ya STY iliyopo karibu na ofisi ya Rais wa Somalia.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya shambulizi hilo vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo viliwadhibiti wanamgambo hao baada ya mapambano yaliyodumu kwa saa saba.

Mapambano hayo ya risasi yalisababisha vifo vya wanajeshi wawili na raia watatu.

Taarifa ya polisi ilisema kuwa wanajeshi wengine wawili na raia tisa walijeruhiwa.

“Vikosi vya usalama pia vimeokoa watu 82 wakiwamo raia pamja na maafisa Serikali,” alisema kamanda wa polisi wa Jiji la Mogadishu, Zakia Hussein Ahmed.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter kamanda Zakia alisema wanamgambo watano walihusika katika shambulizi hilo.

Kundi la wapiganaji wa Al Shabaab limekiri kuhusika na shambulizi hilo.

Akisimulia tukio hilo kamanda Zakia alisema washambuliaji hao walitumia bunduki na mabomu ili kukabiliana na maafisa wa vikosi vya usalama waliofika eeo la tukio kwa ajili ya kudhibiti shambulizi hilo.

Hata hivyo, kamanda Zakia alisema washambuliaji wote watano waliuwa katika mapigano.

“Idadi ya raia waliouawa katika shambulizi hilo inaweza kuongezeka kutona na wengi kujeruhiwa vibaya.”

Kamanda Zakia alisema kwa sasa ulinzi umeimarishwa kwa kuongeza vikosi vya wanajeshi katika barabara inayoelekea katika ofisi Rais.

Hilo ni tukio la pili kwa hoteli hiyo kushambuliwa na magaidi na kusababisha mauaji ya wateja.

Kwa mujibu wa Kituo cha radio cha Dalsalam kilichopo mjini Mogadishu, wabunge wawili pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Somalia Abdulkadir Ali Omar wamejeruhiwa katika shambulizi hilo.