Daktari kupinga ligi Italia kuanza Mei

Muktasari:

Daktari huyo wa magonjwa ya maambukizi anadhani ni mapema mno Ligi Kuu ya Italia, Serie A, kuanza mwishoni mwa mwezi Mei.

Milan, Italia. Daktari maarufu wa Italia aliyebobea katika magonjwa ya maambukizi amesema ataingana na uamuzi waLigi Kuu ya Soka, Serie A, wa kuendela na msimu mwezi ujao.
Mchezo wa soka duniani kote umesimamishwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona ambao umeshachukua maisha ya zaidi ya watu 20,000 nchini Italia.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, ligi hiyo inaweza kuanza mwishoni mwa mweziujao, huku wachezaji wakirejea mazoezini Mei 4.
"Kama ningetakiwa nitoe maoni ya kiufundi, kusema ukweli haitakuwa muda mzuri. Na kwa maana hiyo, itakuwa ni suala la wanasiasa kuamua," alisema Giovanni Rezza, kiongozi wa kitengo cha magonjwa ya Taasisi ya Taifa ya Afya ya Italia.
"Nimesikia baadhi ya watu wakipendekeza kuwepo kwa masharti makali ya uangalizi na wachezaji wakitakiwa kupimwa kila baada ya siku chache. Lakini kuema kweli ni suala ambalo bado liko mbali. Na ni kama tumeshafika mwezi Mei.
"Ni dhahiri kwamba siasa itaamua. Lakini (soka) ni mchezo ambao unahusisha kugusana na kugusana huko kunaweza kumaanisha hatari ya maambukizi."
Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) linatarajiwa kukutana kesho kuzungumzia taratibu za afya, huku uamuzi wa kuzuia watu kutoka katika makazi yao ukiongezwa hadi Mei 3.
"Tutaanza, natumaini, mwanzoni mwa Mei kwa kupima kuhakikisha wachezaji hawana maambukizi na wakati huo mazoezi yanaweza kuanza," rais wa FIGC, Gabriele Gravina aliiambia Sky Sport jana.
Kauli ya Rezza imeshaibua mjadala nchini Italia, huku rais wa klabu ya Torino, Urbano Cairo akisema ni "upuuzi" kufikiria kuanza ligi kabla ya mwisho wa mwezi Mei.
Hata hivyo, Lazio, ambao wako chini ya vinara wa Serie A Juventus kwa tofauti ya pointi moja, alimshambulia Rezza, ambaye ni shabiki wa klabu pinzani ya Roma, akisema kwa utani kuwa angefurahia kuona msimu ukifutwa.
"Itakuwa ni kitu muhimu zaidi kama badala ya kuhofia Lazio kuchukua ubingwa, wamepata njia ya kukabiliana na virusi," alisema msemaji wa Lazio, Arturo Diaconale.
"Ingekuwa pia muhimu kwamba badala ya kutoa hoja zisizotakiwa katika soka, atumie nguvu zake zote kutafiti chanjo inayoweza kuzuia tatizo hilo."