Denmark yaanza kufungua shule

Muktasari:

Serikali imetoa masharti kuwa shule zitakazotaka kufungua lazima ziheshimu kuweka madawati umbali wa angalau mita moja.

Denmark imeanza kufungua shule baada ya kuzifunga kwa muda mrefu kutokana na mlipuko wa virusi vipya vya corona, na hivyo kuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kufanya hivyo.


Shule za chekechea na za msingi zimefunguliwa leo, kwa mujibu wa mwandishi wa AFP, baada ya kufungwa Machi 12 kwa lengo la kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.


Hata hivyo masomo yanarejea katika nusu ya manispaa za Denmark na kwa karibu asilimia 35 ya shule za jijini Copenhagen, kwa kuwa sehemu nyingine zimeomba muda zaidi ili zizoee taratibu za afya ambazo bado zipo.


Shule zote zinatarajiwa zifunguliwe Aprili 20.
Mapema Aprili nchi hiyo ambaye serikali yake ni ya mrengo wa kati ilitangaza kuwa shule zote zitafunguliwa kwa sharti kwamba "kila mtu atakuwa mbali na mwengine na anaosha mikono".


Shule zinatakiwa kuhakikisha kunakuwa na umbali wa mita mbili kati ya madawati darasani na mapumziko yaandaliwe kwa kundi dogo.
Ili kufuata mwongozo huo, shule nyingi zimependelea kuendesha masomo nje ya darasa, hali ambayo ni changamoto kwa shule za mijini.
Baadhi ya wazazi wamepinga kufunguliwa kwa shule, wakieleza hofu ya afya. Mpango wa kupinga suala hilo uliopachikwa jina la "My child is not a guinea pig" umeshavuta saini 18,000.


Henrik Wilhelmsen, mkuu wa shule katika wilaya ya Norrebro, alisema wanategemea "idadi kubwa ya wanafunzi kubakizwa nyumbani."
Shule za kati na za elimu ya juu zitaendelea na masomo kwa njia ya mtandao na zinatarajiwa kufunguliwa Mei 10.
Hadi jana, Denmark ilikuwa imeshathibitisha maambukizi 6,691 ya virusi hivyo na vifo 299.