Jinsi ofisi ya Ruto ilivyotumika kuhalalisha ufisadi

Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto

Nairobi, Kenya. Ofisi ya Makamu wa Rais wa Kenya na wizara ya ulinzi ya nchi hiyo zimetajwa kutumika kuhalalisha ufisadi wa zaidi Sh40 bilioni.

Ufisadi huo uliohusisha kandarasi ya ununuzi wa vifaa vya kijeshi vyenye thamani ya Sh40 bilioni za Kenya unadaiwa kufanywa na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa.

Alhamisi iliyopita waziri huyo alikamatwa kufuatia agizo la Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI), George Kinoti.

Waziri huyo aliyelala rumande kwa siku tatu, jana alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya utapeli wa ununuzi wa vifaa vya kijeshi. Hata hivyo, waziri huyo alipewa dhamana kwa masharti ya kuwasilisha fedha taslimu Sh1 milioni karibu shilingi 22 milioni za kitanzania.

Awali DCI Kinoti alidai kuwa waziri huyo wa michezo akitumia ofisi hizo nyeti ikiwamo ya Makamu wa Rais, Dk William Ruto kuwarubuni wawekezaji kutoka nchini Marekani.

Alisema picha za CCTV zilizochukuliwa kwenye ofisi ya makamu wa rais zinaonyesha wasaidizi wa Ruto wakiwa kwenye mkutano uliofanyika Februari 13 na waziri huyo wa zamani pamoja na wawekezaji hao.

Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ruto amekiri ofisi yake ilitumika na waziri huyo pamoja na wawekezaji hao watatu lakini hakufahamu kilichokuwa kikiendelea.

Ruto alisema hizo ni njama za kuhujumu azma yake ya uchaguzi mkuu ujao vitendo vinavyofanywa na mahasimu wake.

Waziri wa Ulinzi, Monica Juma alisema hakuwahi kutia sahihi nyaraka zozote na wawekezaji hao na kwamba ilighushiwa.

Waziri Echesa anadaiwa kupokea kiasi hicho cha fedha kwa lengo la kuwaunganisha wawekezaji hao na watu wanaohusika kutoa zabuni ya vifaa vya kijeshi.