Mwili wa Mugabe warejeshwa nyumbani kwake Harare

Muktasari:

  • Ni baada ya kufanyiwa sherehe za kimila iliyoendeshwa na viongozi wa ukoo na kimila wakiwamo machifu kijijini kwake Kutama alipozaliwa kiongozi huyo.

Harare. Zimbambwe. Mwili wa Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe umerejeshwa nyumbani kwake mjini Harare siku moja baada ya kufanyiwa sherehe za kimila.
Mwili wa Mugabe uliwasili nyumbani kwake jana ukitokea Kutama umbali wa kilometa 90 kuelekea Magharibi wa nchi hiyo ambako ndipo alipozaliwa. Jumatatu iliyopita wanakijiji walitoa heshima za mwisho na kufuatiwa na shughuli ya kimila iliyoendeshwa na viongozi wa ukoo na kimila wakiwamo machifu.
Mwili wa Mugabe ulilala kijijini hapo Jumane iliyopita  kisha kurejeshwa nyumbani jana kwake mjini Harare kwa ajili ya kihifadhiwa.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya mazishi ya kitaifa yaliyofanyika Jumamosi na kuhudhuriwa na maelfu ya watu wakiwamo viongozi kadhaa wa Afrika.
Awali akizunguza na Shirika la habari la AFP, mjukuu wa kiongozi huyo, Leo Mugabe alisema ingawa tarehe rasmi ya mazishi haijapangwa lakini familia imekubaliana kumzika baada ya mwezi mmoja.
Mjukuu huyo alisema kuwa katika kipindi chote cha mwezi mmoja mwili wa kiongozi huyo utahifadhiwa nyumbani mjini Harare.
Mjukuu huyo alisema mwili huo utazikwa mwezi ujao katika makaburi ya kitaifa ya mashujaa, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kaburi lake.