Trump aongeza vikwazo Iran, kambi zalipuliwa

New York. Rais wa Marekani, Donaldo Trump ametangaza kuiongezea Iran vikwazo vya kiuchumi kama nchi hiyo haitabadili tabia zake.

Trump alitoa kauli hiyo jana wakati akilihutubia Taifa hilo baada ya taarifa ya Iran kushambulia kwa makombora kambi mbili tofauti zinazotumiwa na vikosi vya Marekani nchini Iraq.

Katika hotuba yake Rais Trump alisema Marekani iko salama na shambulio la Iran halijawa na madhara kwao.

Makombora hayo yalishambulia kambi ya Ain-Asad iliyopo jimbo la Anbar na kambi nyingine ya Erbil jana na hivyo kuongeza uhasama kati ya Marekani na Iran baada ya vikosi vya Marekani kumuua kamanda wa jeshi la Iran, Jenerali Qassem Soleimani.

Iran iliapa kulipiza kisasi baada ya kuuawa kwa watu wake muhimu na shambulizi lao lilichukuliwa kama kisasi cha Iran kwa Marekani kama walivyoahidi viongozi wake mara kadhaa wakati wa msiba wa Soleimani.

Katika taarifa yake, jeshi la Iraq lilithibitisha kutokea kwa mashambulizi 22 katika kambi zilizopo Anbar na Erbil nchini humo.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba makombora 17 yaliilenga kambi ya Ain al-Asad wakati makombora matano yakielekezwa kambi ya Erbil ambayo ni kambi ya muungano wa majeshi kutoka nchi mbalimbali.

Hata hivyo, wamedai kwamba hakuna kifo wala majeruhi kwa upande wa vikosi vya jeshi la Iraq.

Norway na Denmar nazo zimetoa taarifa kwamba hakuna askari wao hata mmoja aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulizi hilo lililotekelezwa na Iran, msemaji wa jeshi la Norway, Brynjar Stordal alinukuliwa na shirika la habari la Reuters. Amesema nchi yake ina askari 70 nchini Iraq.

Denmark ina askari 130 katika kambi hiyo ambayo imeunganisha askari kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kupambana na kikundi cha magaidi cha Islamic State (Isis).

Hata hivyo, kituo cha televisheni ya Taifa cha Iran kilitangaza kwamba takribani askari 80 wa Marekani walikufa katika shambulizi hilo.

Akimzungumzia Jenerali Soleimani, Trump alisema kwamba jenerali huyo katika siku za karibuni alikuwa amepanga mashambulizi mapya dhidi ya Wamarekani lakini wamemdhibiti.

Zaidi ya hilo, Trump pia alisisitiza kwamba kwa wakati huu akiwa Rais wa Marekani, Iran kamwe haitoruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia.

Miongoni mwa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Iran ni pamoja na marufuku ya kushirikiana na kampuni za Iran zinazohusika na biashara ya usafiri wa anga ambazo haziruhusiwi kununua ndege pamoja na vifaa vya kukarabati ndege.