Uchunguzi wa miaka 34 mauaji ya waziri mkuu kukamilika Juni

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Sweden, Olof Palme.

Stockholm, Sweden. Uchunguzi wa mauaji ya Waziri Mkuu wa Sweden, Olof Palme yaliyofanyika miaka 34 iliyopita, utakamilika ndani ya miezi michache, ukiashiria mwisho wa kitendawili cha muda mrefu kilichoisumbua nchi.

Waendesha mashtaka ama “watafungua mashtaka au kufunga uchunguzi,” alisema Krister Petersson, ambaye anaongoza timu iliyoundwa kuchunguza suala hilo alipoongea na AFP, akiongeza kuwa kuna uwezekano matokeo hayo yakatangazwa mwishoni mwa mwezi Juni.

Palme aliuawa Februari 28, 1986, baada ya kutoka jumba la sinema akiwa na mkewe, Lisbet jijini Stockholm. Siku hiyo jioni alikuwa amemruhusu mlinzi wake aondoke.

Mtu ambaye hakujulikana alimsogelea na kumpiga Palme risasi ya mgongoni, akimuacha kiongozi huyo, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 59, akilala pembeni ya dimbwi la damu.

Katika maadhimisho ya miaka 30 ya uhalifu huo, Waziri Mkuu wa sasa, Stefan Lofven aliyaita mauaji hayo kuwa ni “kidonda cha wazi”.

“Nadhani nchi nzima, na bila shaka, familia inataka kuona mwisho,” alisema Lofven alipoongea na gazeti la Aftonbladet jana.

“Tumekuwa tukitafuta suluhisho kwa muda mrefu,” aliongeza.

Zaidi ya watu 10,000 wamehojiwa, na kati yao 134 wamedai kuhusika, na mafaili ya kesi hiyo yamewekwa makabatini yenye nafasi ya urefu wa mita 250, sawa na viwanja viwili vya mpira wa miguu.

Christer Pettersson, aliyezoea uhalifu mdogomdogo na anayetumia dawa za kulevya, alihukumiwa kuhusika na kifo hicho Julai mwaka 1989 baada ya Lisbet kumtambua katika gwaride la utambulisho lililokosolewa na watu kadhaa.

Lakini aliachiwa huru miezi kadhaa baadaye na mahakama ya rufaa ambayo ilikataa ushahidi wa Lisbet. Pettersson alifariki mwaka 2004 wakati mjane wa Palme alifariki mwaka 2018.

Kwa miaka kadhaa, wachunguzi wamehusisha mauaji hayo na kundi la Kikurdi la waasi wa Uturuki la PKK, Jeshi la Sweden na polisi, na Idara ya Ujasusi ya Afrika Kusini.

Jana, wataalamu kadhaa na waandishi wa safu za maoni walisema kuwa suala hilo linaweza kufungwa kwa kuwa wote wanaotuhumiwa wameshafariki.