Wanasiasa zamu yao imekwisha, leo ni siku ya majaji milioni 29

Muktasari:

Watanzania milioni 29.188 leo wanatarajia wanapiga kura kuchagua viongozi wao wa watakaowahudumia kwa miaka mitano ijayo. Kuanzia rais, wabunge na madiwani. Zanzibar walianza jana kuchagua rais na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Watanzania milioni 29.188 leo wanatarajia wanapiga kura kuchagua viongozi wao wa watakaowahudumia kwa miaka mitano ijayo. Kuanzia rais, wabunge na madiwani. Zanzibar walianza jana kuchagua rais na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Leo unafanyika uchaguzi baada ya kupita siku 63 za kampeni. Vyama 19 vya siasa vimesimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali. Vyama 15 vinagombea urais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vyama 17 vinashindania kiti cha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Wagombea wameshajinadi, leo ni siku ya wananchi kuamua. Hapa ndipo kwenye utamu wenyewe. Kwamba wanasiasa wamekuwa na fursa pana ya kujinadi kwa kila mbinu, maarifa na uhuru. Zamu yao iliisha jana. Leo wananchi wanaamua. Kila mpiga kura kwa utashi wake anamchagua yule aliyemshawishi.

Hapo ndipo unapata mantiki ya kwamba uchaguzi ni mali ya watu. Mwisho kabisa wao ndio wanaamua nani awe kiongozi wao. Hilo linafaa kuwepo akilini kwa kila mwanasiasa kuwa majukumu yao yalikuwa kuomba ridhaa ya vyama vyao ili wasimamaishwe kugombea, baada ya hapo kutimiza vigezo vya tume, kisha kufanya kampeni. Kuhusu nani atashinda, huo ni uamuzi wa wananchi.

Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln alipata kusema: “Uchaguzi ni mali ya watu, kama wao wenyewe watageuza migongo na kukalia moto, ni wao wenyewe watakaolazimika kukaa kwenye makalio yaliyojeruhiwa na moto.” Alimaanisha kuwa uchaguzi ni mali ya watu, kama watachagua vibaya ni wao watakaoumia.

Sasa, wakati tukiomba uchaguzi uende salama na uishe kwa amani, ni wajibu kuwakumbusha wanasiasa kuheshimu uamuzi wa wananchi. Tena wanasiasa wa Tanzania wanapaswa kujifunza kwa mfano wa karibu zaidi, kutoka nchi ndogo yenye watu wasiofikia 100,000, Shelisheli.

Oktoba 22, mwaka huu, Shelisheli walianza kufanya uchaguzi wa Rais. Walikamilisha Oktoba 24 (juzi). Kiongozi wa chama cha Seychelles Democratic Alliance, Wavel Ramkalawan, ameshinda. Ramkalawan, mchungaji wa Anglican, alimshinda Rais Danny Faure. Kabla ya ushindi huo, Father Ramkalawan alishagombea urais wa Shelisheli mara sita bila mafanikio. Ya saba kashinda.

Shelisheli ilipata uhuru mwaka 1977, ikawa chini ya mfumo wa chama kimoja. Mwaka 1993 ilikaribisha mfumo wa vyama vingi. Wakati huo wote, chama tawala cha United People’s Party ambacho sasa kinaitwa United Seychelles Party, kikawa kinashinda. Safari hii imekuwa mara ya kwanza kwa chama cha upinzani kushinda mamlaka ya Serikali Shelisheli tangu uhuru.

Baada ya matokeo kutangazwa, Ramkalawan na Rais Faure, walitokeza mbele ya vyombo vya habari pamoja. Ramkalawan akasema: “Mimi na Faure ni marafiki wa karibu. Uchaguzi sio mwisho wa mchango wa kila mmoja kwenye nchi yake. Katika uchaguzi huu hatukuwa na mshindi wala mshindwa. Mshindi wa jumla wa uchaguzi huu ni nchi yetu, Shelisheli.” Wakati Father Ramkalawan akisema hayo, Rais Faure alikuwa akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na kilichosemwa.

Kipindi hiki ambacho dunia ipo kwenye harakati za uchaguzi katika nchi nyingi, tunashuhudia visa vya chuki na siasa za kung’ang’ania madaraka, Faure na Ramkalawan wanaionesha dunia kwamba uchaguzi ni kwa ajili ya nchi. Kukubali matokeo inawezekana. Mshindi na mshindwa wanaweza kupeana mikono kwa upendo.

Kipidi hiki Guinea na Ivory Coast wanahesabu idadi ya watu waliopoteza maisha kisa uchaguzi. Rais Donald Trump akigoma kutamka kuwa akishindwa uchaguzi ataachia madaraka. Rais Faure na Ramkalawan wanaipa somo kubwa dunia.

Faure na Ramkalawan ni somo pia kwa Tanzania. Yapo mazingira na zipo kauli tata zilizotoka sana kipindi cha kampeni. Tanzania ni nchi kubwa. Tunahitaji siasa za heshima, zenye utii wa demokrasia. Wananchi ndio waamuzi kesho yao na leo wanafanya kile ambacho Katiba inataka wafanye. Wanasiasa wanatakiwa kuheshimu mchakato bila kuingilia, kisha waheshimu matokeo.

Kama alivyosema Ramkalawan, katika uchaguzi hakuna mwanasiasa atakayeshindwa, bali mshindi wa jumla ni mwananchi. Maana ndiye anayechagua. Uchaguzi wa Tanzania si wa tume, kama maana ya NEC wala ZEC, si wa polisi wala jumuiya ya kimataifa. Ni wa Watanzania. Kama Watanzania wenyewe watakosea, ni wao wakaoishi katika uongozi mbaya.

Mwaka 1997, katika uchaguzi wa Liberia, vijana walionywa wasimchague Charles Taylor kwa sababu aliendesha vita vya kiraia vilivyoua wananchi wengi. Zaidi ya watu 620,000 walipoteza maisha. Vijana wakaanzishaa kauli mbiu “He Killed My Ma, He Killed My Pa, I Vote for Him” – “Alimuua Mama, Alimuua Baba, Nitamchagua”. Taylor alishinda, kisha Liberia wakajuta. Walijuta wao.