Wawili wapigwa risasi Uganda kukiuka amri ya Rais Museveni

Muktasari:

Rais wa Uganda, Yoweri Mseveni amepiga marufuku usafiri wa umma katika mapambano ya kuenea kwa virusi vya corona nchini humo.

Kampala. Watu wawili wamefikishwa hospitali baada ya kupigwa risasi na maofisa wa polisi wanaosimamia utekelezaji wa amri ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ya kusitisha usafiri wa umma ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona nchini humo.

Alex Oryem na Kasim Ssebude ambao wamelazwa katika hospitali ya Mukono, walipigwa risasi wakati wanaendesha bodaboda zao katika manispaa ya Mukono nchini humo.

Oryem alipigwa risasi mguuni wakati Ssebude alipigwa risasi tumboni. Vijana hao ambao wanafanya kazi za ujenzi, walikuwa wakitoka Seeta kwenda Namugongo kabla ya kuvamiwa na polisi kwa madai ya kukiuka amri ya Rais Museveni.

Oryem alilieleza gazeti la Daily Monitor nchini humo kwamba hakujua maelekezo yaliyotolewa na Rais Museveni kwa sababu hakutazama televisheni Jumatano usiku wakati Rais Museveni alitangaza hatua za kukabiliana na virusi vya corona.

Rais Museveni alisema bodaboda wasiachwe wasafirishe abiria kwa kutumia usafiri huo.

“Wakati tunakwenda kazini, tulikutana na maofisa wawili wa polisi ambao walituzuia kwa madai kwamba tulikuwa wawili kwenye pikipiki. Tulipojaribu kuuliza kosa tulilolifanya, walianza kutupiga risasi,” alisema.

Alisema maofisa wa polisi walianza kwa kupiga risasi hewani kabla ya kuwapiga wao.

Msemaji wa jeshi la polisi katika mji wa Kampala, Patrick Onyango alisema vijana hao walipigwa risasi baada ya kujaribu kumshambulia ofisa wa polisi.

“Baada ya polisi kuwasimamisha, walijaribu kuwashambulia maofisa wetu. Alipiga risasi hewani kama onyo. Watu wasipuuze maelekezo ya Rais yenye lengo la kuzuia kuenea kwa virusi vya corona nchini Uganda,” alisema.

Mpaka sasa Uganda imethibitisha maambukizi 18 ya virusi vya corona huku watu wengine 197 wakipimwa maambukizi ya ugonjwa huo na kuwekwa kwenye karantini ili kama wameambukizwa wasiweze kuambukiza wengine.