Wiki mbaya kwa Rais Trump

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni wiki mbaya kwa Rais wa Marekani, Donald Trump kutokana na jinsi alivyobanwa na tuhuma mbalimbali.

Trump, kiongozi machachari ameingia katika tuhuma nzito za kufanya mazungumzo ya siri na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ili kumchunguza mpinzani wake Joe Biden.

Chama cha Democrats kinamtuhumu Trump kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kutumia msaada wa kijeshi na Ikulu ya White House, kumshinikiza Rais huyo kufungua upelelezi dhidi ya Biden na mwanaye Hunter.

Kijana huyo wa Biden alifanya kazi katika bodi ya kampuni moja ya gesi nchini Ukraine iitwayo Burisma.

Ingawa Trump mwenyewe ameonyesha kutojali tuhuma hizo na kuungwa mkono na wabunge wa chama cha Republican, ukweli ni kwamba madai hayo yanaweza kumng’oa madarakani.

Jumatano iliyopita Bunge la Marekani chini ya Spika wa Bunge la nchi hiyo, Nancy Pelosi aliyetangaza mpango wa kumng’oa madarakani kiongozi huyo, lilianzisha uchunguzi wa kina na wazi.

Wakati tuhuma hizo zikiendelea kutikisa, kiongozi huyo amejikuta katika wakati mgumu baada ya Mahakama ya Rufaa nchini humo kutoa ruksa kwa Bunge kuagiza nyaraka zake za kodi za karibu miaka 10 kwa ajili ya ukaguzi.

Uamuzi huo umezima juhudi za Trump ambaye amekuwa akipambana kuhakikisha rekodi zake za kibiashara haziangukii mikononi mwa wapinzani wake wa Democrats.

Hii ni mara ya pili kwa Trump kukwama katika Mahakama Kuu katika jaribio la kuzuia wito wa Bunge wa kutaka nyaraka za zaidi ya miaka minane ya ulipaji kodi.

Trump akata rufaa

Ijumaa iliyopita kiongozi huyo aliwasilisha pingamizi lake katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufani nchini humo kutoa ruksa kwa Bunge kuagiza nyaraka zake kodi za kwa ajili ya ukaguzi.

Hatua hiyo imefikiwa siku moja baada ya uamuzi huo ambako wakili wa Trump, Jay Sekulow alitangaza kuwa jopo la wanasheria binafsi wa Rais huyo litakata rufaa katika Mahakama ya Juu.

Awali majaji katika Mahakama ya Rufani waliyakataa maombi ya Trump ya kutaka kusikiliza upya uamuzi uliofanywa na majaji watatu mwezi uliopita.

Katika uamuzi huo wa Oktoba, pia majaji walikataa maombi ya Trump kwa uwiano majaji wawili kukayataa na mmoja kuyakubali, hivyo kuipa kamati ya Bunge mamlaka ya kumtaka Rais kuwasilisha nyaraka za kodi.

Bunge linaloongozwa na Democrats linataka nyaraka za ulipaji kodi wa Trump kati ya 2011 na 2018, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa biashara zake kwa kuwa aliahidi kwenye kampeni kuwa angetoa rekodi hizo.

Wanasheria wanataka kubaini iwapo Trump alipandisha thamani ya mali zake ili kupata mikopo.

Katika wito wa Bunge wa Aprili, Trump alitakiwa kuwasilisha taarifa za hali ya kifedha, ripoti za mwaka na za kila mara za fedha, ripoti za ukaguzi huru wa hesabu na ukaguzi uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya Mazars.

Ikulu ya Marekani ambayo imeueleza uchunguzi huo kama unyanyasaji kwa Rais, imesema Bunge halihitaji nyaraka hizo ili kufanikisha majukumu yake kama chombo cha kuitunga sheria.

Mmoja wa wagombea wa Demokratic katika uchaguzi mwaka 2020, Joe Biden alifurahia uamuzi wa Mahakama ya Rufani, akisema kupitia Twitter, kuwa Wamarekani anapaswa kujua “Trump anachoficha katika nyaraka za kodi.”

Mabalozi wanne watoa ushahidi

Jumla ya mabalozi wanne Marekani wamekwishatoa ushahidi mzito yakiwamo maelezo mapya kuhusu juhudi za Rais huyo kuitaka Ukraine kumchunguza mshindani wake katika uchaguzi wa 2020, Joe Biden.

Ushahidi huo wa wazi umetolewa na kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni, kuanzia Jumatano iliyopita katika kamati ya Bunge inayoendesha uchunguzi wa dhidi ya Trump.

Hata hivyo, Rais Trump mara kadhaa amepuuza uchunguzi huo unaosimamiwa na Bunge linaoongozwa na Chama cha Democrats, kuwa ni “kutafuta mchawi” na kuwa ana kazi nyingi hivyo hawezi hata kufuatilia mahojiano hayo.

William Taylor, balozi mwandamizi wa Marekani nchini Ukraine, alianza kutoa ushahidi wake mbele ya Kamati ya uchunguzi akieleza masuala mapya kuhusu juhudi za Trump kushinikiza Ukraine, hoja ambayo ndiyo msingi katika mchakato huo wanne, wa kutaka kumng’oa rais katika historia ya Marekani.

Ushahidi muhimu ni maelezo ya simu ya Ikulu ya Julai 25 kati ya Trump na Zelensky ambapo Trump anamtaka mwenzake wa Ukraine amchunguze Biden.

Taylor aliileza kamati hiyo kuwa Trump alikuwa anajali zaidi uchunguzi (dhidi ya Buden) kuliko alivyokuwa anaijali Ukraine.

Mwanajeshi huyo wa zamani na mwanadiplomasia mkongwe, ambaye pia alitoa ushahidi wa siri mwezi uliopita amesema kuwa alifahamu kuhusu mawasiliano hayo ya simu kati Trump na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Ulaya, Gordon Sondland kwa kuwa mmoja wa wafanyakazi katika ofisi yake aliyasikia.

Mfanyakazi huyo alimuuliza Sondland baada ya simu kuhusu nini Trump alikuwa anafikiria kuhusu Ukraine na kuambiwa kuwa “alikuwa anajali kumchunguza Biden na mwanaye,” alisema Taylor.

Balozi mwingine wa zamani wa Marekani nchini Ukraine, Marie Yovanovitch naye ametoa ushahidi wake Ijumaa katika siku ya pili ya kusikilizwa hadharani ushahidi unaoweza kupelekea kufunguliwa mashtaka na kuondolewa madarakani kwa Rais Trump.

Wakati wa ushahidi wake mbele ya Kamati ya Bunge ya Ujasusi, Rais Trump alikuwa kwenye mtandao wa Twitter akimshambulia mwanadiplomasia huyo na rekodi yake.

Aliandika kuwa kila mahali alikofanya kazi Marie Yovanovitch mambo yalikwenda mrama. Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Adam Schiff aliisoma kauli hiyo ya Trump kwa Yovanovitch wakati wa kikao hicho, akimuuliza jibu lake.

“Siwezi kuzungumzia kile rais anajaribu kukifanya, lakini nadhani athari ni kutisha,” alisema.

Marie anayefahamika kwa rekodi yake ya kupambana na rushwa, alipelekwa Ukraine 2016 ambako alihudumu kama balozi wa Marekani hadi alipolazimika kuondoka Mei 2019. Schiff alisema kuondolewa kwake kulisaidia kuweka mazingira ya kufunguliwa njia isiyo rasmi ya kuendesha sera ya Ukraine ambayo ilitumiwa na Trump na washirika wake kuishinikiza nchi hiyo kuwachunguza wapinzani wa kisiasa wa rais huyo.

Balozi Davis Holmes ambaye alisikiliza mazungumzo baina ya kiongozi huyo wa Marekani na Rais wa Ukraine naye ametoa ushahidi wake ili kufanikisha uchunguzi huo.