“Zaidi ya waandamanaji 100 wameuawa Iran”

Wednesday November 20 2019

London, Uingereza. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema kuwa zaidi ya watu 100 wameuawa wakati wa machafuko yaliyozuka wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika hilo, maaji hayo yamehusisha wananchi katika miji 21 ambao walikuwa wakipinga kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol.

Katika ripoti yake iliyotolewa jana Jumanne Novemba 19, shirika hilo limesema kuwa polisi wa kulenga shabaha waliwafyatulia risasi za moto makundi ya waandamanaji kutoka juu ya majengo.

“Watu wengi walipoteza maisha katika tukio la polisi kuwafyatulia risasi wakiwa ndani ya helikopta,”

Shirika hilo lenye makao yake mjini London limesema taarifa hiyo ni kwa mujibu wa duru za kuaminika na vyanzo vingine ikiwamo mashuhuda, kanda za video na maelezo ya watetezi wa haki za raia.

Amnesty pia ilisema vikosi vya polisi na intelejensia havikurudisha miili ya waliuawa kwa familia zao na vimelazimisha baadhi ya miili kuzikwa haraka bila kufanyiwa uchunguzi wa kitababu.

Advertisement

Taarifa hiyo imefichua jinsi vikosi vya usalama nchini Iran vinavyoendesha mauaji ya raia kinyume na sheria ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu katili na nguvu iliyopindukia.

Raha Behreini, ambaye ni mwanasheria na mtafiti wa Amnesty International alisema “mamlaka za Iran zina historia ya kutumia ukatili na nguvu kubwa dhidi ya wale wanatimiza haki yao ya kujieleza na kuandamana kwa amani.

Hata hivyo, inaonekana kwa sasa wamezidisha zaidi ukandamizaji kwa sababu hawataki maandamano hayo yawe makubwa”

Katika hatua nyingine, mamlaka nchini humo zimezima huduma za mtandao wa intaneti tangu Jumamosi iliyopita.

Kukosekana kwa upatikanaji taarifa kumevifanya vyombo vya habari vya Iran na maafisa wa nchi hiyo pekee kuwa na uwezo wa kutoa taarifa kuhusu kinachoendelea.

Afisa mmoja nchini Iran amesema maandamano hayo yamepungua nguvu baada ya kikosi cha ulinzi wa mapinduzi cha Jeshi la Iran kutishia kuchukua hatua kali iwapo yataendelea.

Maandamano dhidi ya serikali nchini Iran yalianza Ijumaa iliyopita baada ya tangazo la kupandishwa kwa bei za mafuta kwa asilimia 50.

Kupanda kwa bei ya mafuta kunamaanisha kuwa changamoto nyingine kwa raia wa nchi hiyo ambao tayari wameathiriwa na kuanguka kwa sarafu ya nchi hiyo.

Hali imezidi kuwa mbaya nchini humo tangu utawala wa Rais Donald Trump kuitoa Marekani kutoka mkataba wa nyuklia wa Iran na madola yenye nguvu na kurejesha vikwazo vinavyoulemeza uchumi wa Iran.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani aliahidi kuwa nyongeza ya bei ya mafuta itatumika kutoa ruzuku na marupurupu zaidi kwa familia masikini. Hata hivyo, uamuzi huo umezusha hasira kubwa miongoni mwa raia wa Taifa hilo la Kiislam.

Advertisement