Asilimi 95 ya wahudumu wa afya Uganda hawanawi mikono

Muktasari:

Utafifiti uliofanywa na Shirika la WaterAid katika jiji la Kampala umebainisha kwamba asilimia 95.6 ya watoa huduma za afya hawaoshi mikono yao kwa sababu ya kukosekana kwa sabuni na maji

Kampala, Uganda. Asilimia 95.6 ya watumishi katika vituo vya afya mjini Kampala hawaoshi mikono yao wakati wa kazi, utafiti umebainisha.

Utafiti huo uliofanywa na Shirika la WaterAid katika kipindi cha Novemba mwaka jana na Julai mwaka huu, umebainisha kwamba watoa huduma za afya 44 kati ya 46 kutoka katika vituo vya afya 63 vilivyofanyiwa utafiti huo jijini Kampala walisema hawaoshi mikono yao.

Akizindua ripoti ya utafiti huo, Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid, Jane Sembuche alisema lengo ni kuangalia hali ya upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira katika vituo vya afya.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 65 ya watoa huduma za afya hawaoshi mikoni yao kwa sababu hawana sabuni wakati asilimia 41 wakisema ni kukosekana kwa maji katika vituo vyao.

Ripoti hiyo imebainisha pia kwamba asilimia 40 ya vituo vya afya havina usimamizi wa takataka, jambo ambalo linaviweka asilimia 60 katika hali hatarishi ya kupata maambukizi kutokana na uchafu.

Mwakilishi wa Jeshi la Wananchi wa Uganda (UPDF) bungeni, Kanali Felix Kulayigye alinukuliwa na gazeti la Daily Monitor akisema “matokeo ya utafiti huo ni sahihi lakini yanatoa tahadhari. Kama haya ni matokeo kwa Kampala na maeneo ya jirani, basi hali ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini.”

Kulayigye alilalamikia tabia mbaya na uchafu wa watoa huduma za afya na kutaka wawekewe vikwazo katika kutoa huduma hiyo.

Utafiti huo pia ulibaini kwamba asilimia 78 ya vituo vya afya vinategemea maji ya bomba, 17 maji ya mvua, tatu visima vya kuchimba wakati wakati asilimia moja wanatumia maji ya visima virefu na kwenye matenki.

“Nimeguswa kwamba asilimia 78 ya vituo vya afya ndani ya Kampala ndiyo vinatumia maji ya bomba. Siyo habari njema kwamba asilimia 22 wanatumia maji ya mvua, visima vya kawaida na visima virefu, hiyo ni mbaya sana,” alisisitiza David Kateeba kutoka Mfuko wa Mazingira wa Uganda.