Wasanii Nigeria mfano wa nguvu ya sanaa katika kulinda demokrasia

Muktasari:

Jumanne ya wiki iliyopita, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, alikifutilia mbali Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS) cha Jeshi la Polisi Nigeria, na kuagiza maofisa wote wa kikosi hicho wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu wafukuzwe kazi.

Jumanne ya wiki iliyopita, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, alikifutilia mbali Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS) cha Jeshi la Polisi Nigeria, na kuagiza maofisa wote wa kikosi hicho wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu wafukuzwe kazi.

Buhari alitoa amri hiyo kama kutekeleza sauti ya umma. Wanigeria kwa makundi, wasanii maarufu, wanaharakati na wananchi wa kawaida, walitokeza barabarani kushinikiza SARS ifutwe. Ni baada ya kikosi hicho kubainika kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu.

Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nigeria, Mohammed Adamu, aliwapiga marufuku maofisa wa SARS kusimamisha magari na kufanya ukaguzi. Wananchi wakasema uamuzi huo wa IGP Adamu haukutosheleza. Kilochotakiwa ni SARS kuvunjwa, baada ya kubainika walikuwa wakihusika na matendo ya uhalifu.

Tangu mwaka 2016, Shirika la Kimataifa la utetezi wa haki za binadamu, Amnesty International, limekuwa likichapisha ripoti kuonesha kuwa SARS walikuwa wakitesa watu, wakipora mali zao na hata kuwaua kwa kuwapiga risasi kwa kisingizio kwamba ni majambazi.

Kwa nyakati tofauti ripoti za Amnesty International zilionyesha kuwa SARS walikuwa wakisimamisha magari, wanafanya ukaguzi, kwa kigezo cha kupambana na uhalifu, kisha wanashinikiza kupewa rushwa, vilevile kupiga, kutesa na hata kuua watu wasio na hatia.

Amnesty international pia waliandika kuwa SARS wamekuwa wakijitajirisha kwa njia ya uhalifu, vilevile wakiwaua watu wanaowatuhumu kuwa majambazi bila kuwafikisha mahakamani.

Hivi karibuni, Amnesty International walitoa video iliyoonesha kijana wa Kinigeria akipigwa risasi na maofisa wa SARS. Ni video hiyo ndio iliyoibua hisia za watu wengi na kuingia barabarani kutaka ivunjwe. Hatimaye kikosi hicho kilivunjwa.

Kuna somo kwa wasanii wa Tanzania. Kujitokeza katika mambo nyeti ya nchi bila woga. Nigeria, wasanii wote maarufu walishiriki harakati za kushinikiza SARS ivunjwe. Na hatimaye, sauti zao zilisikika. Na sasa, wasanii hao wamekuwa wakiendelea kuongoza maandamano kutaka ukatili wa polisi ukome.

Inawezekana shinikizo lisingepata nguvu kama wasanii Nigeria wasingejitokeza. Wasanii wana nguvu kubwa, kama wataamua kuitumia. Maandamano yalipoanza yalionekana kuwa na nguvu ndogo. Hata hivyo, kitendo cha wasanii kujitokeza barabarani na kuongoza maandamano, kilibadili upepo. Maelfu waliingia mtaani kutaka mabadiliko.

Ni kweli, agenda ya SARS imekuwa ikitanuka. Kutoka kikosi hicho kuvunjwa hadi kutokomeza ukatili wa kipolisi kwa rais. Mara, kuna waandamanaji wanaopaza sauti kwamba umewadia wakati wa kutokomeza utawala mbaya. Awali walibeba mabango yaliyosema “EndSars”, kisha “EndPoliceBrutality”, sasa wananadi “EndBadGovernance”.

Kuna watu wanaamini yanayotokea Nigeria kuna mkono mkubwa kisiasa. Wapo wanaowatuhumu wasanii maarufu wa nchi hiyo kwamba wanatumiwa na wanasiasa, hususan wapinzani wa Rais Buhari. Lakini lipo swali; je, wasanii waliingia barabarani kuongoza maandamano pasipo sababu ya msingi?

Ripoti ya Amnesty Internation na video iliyotolewa, ilifichua kila kitu. Hivyo, wasanii walikuwa na sababu ya msingi kabisa ya kuingia barabarani kutaka mabadiliko ya kimfumo katika jeshi la polisi la nchi yao. Kama kuna wanasiasa wametumia mwanya huo kuingiza agenda zao dhidi ya Rais Buhari, basi watakuwa wamecheza karata yao kwa sayansi ya hali ya juu.

Mathalan, mwanamuziki David Adeleke ‘Davido’, aliingia barabarani na kuongoza kadamnasi kushinikiza SARS wafutwe. Davido anatokea familia yenye nguvu kubwa ya kisiasa Nigeria, hususan jimbo la Osun. Ni wanachama wa chama cha PDP kinachopingana kwa ukaribu na APC cha Buhari.

Hata uchaguzi uliopita, Davido alifanya kampeni waziwazi kukipigania chama cha PDP ili kishinde na kumwangusha Buhari na APC yake. Hivyo, lipo eneo ambalo halibishaniwi, kwamba Davido ni mpinzani kisiasa dhidi ya Buhari. Na hiyo ni ndani kabisa ya familia yake.

Pamoja na hivyo, cha kutazama ni nguvu ya sanaa pale wasanii wanapoamua mabadiliko yatokee. Wasanii wa Tanzania nao wanayo nafasi ya kujifunza ili yenye kupaswa kutokea yatokee kwa nguvu zao. Ni uamuzi wao tu.

Haya ni maoni binafsi ya mwandishi wa uchambuzi huu