Ajali ya ndege yaua watu 176 Iran

Muktasari:

Wakati mzozo kati ya Iran na Marekani ukiendelea huko Mashariki ya Kati, ndege aina ya Boeing 737-800 imeanguka Tehran, Iran na kuua watu 176 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo. Chanzo cha ajali hiyo kinatajwa kuwa ni hitilafu za kiufundi.

Kiev. Ndege ya Shirika la Ndege la Kimataifa la Ukraine (UIA) Boeing 737-800 imeanguka huko Iran leo Januari 8 na kuua watu wote 176 waliokuwa kwenye ndege hiyo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy amethibitisha.

Chanzo cha ajali hiyo hakijaweza kubainika mara moja ingawa maofisa wa Iran wanasema imesababishwa na matatizo ya kiufundi bila kubainisha wazi ni matatizo gani hayo.

Hiyo ni ajali ya kwanza kwa shirika la UIA ambalo lilianzishwa mwaka 1992 baada ya kuanguka kwa muungano wa Kisovieti. Ndege hiyo imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya kiufundi kwa miaka kadhaa, hata hivyo haikuwahi kuanguka.

UIA imeeleza kwenye tovuti yake kwamba ilipewa cheti cha usalama na Chama cha Kimataifa cha Usafariri wa Anga (IATA), ikimaanisha kwamba operesheni zake na viwango vya usalama vilikidhi viwango vya kimataifa.

Shirika hilo linalofanya safari za ndani na kimataifa ina ndege 42 ambazo kwa mujibu wa tovuti yake inajumuisha ndege mbalimbali za Boeing zikiwemo 737-800 na 737-900.  Pia, inaendesha ndege aina ya Embraer.

Tatizo la kifedha ndiyo lilisababisha shirika hilo kupunguza mtandao wa safari zake mwaka jana.

UIA iko katika mchakato wa kuboresha safari zake na tayari imeagiza ndege tatu aina ya Boeing 737 Max. Hata hivyo, aina hiyo ya ndege hazijaanza kutolewa kwa sababu za kiusalama hasa baada ya mfululizo wa ajali mwaka uliopita.