Al Shabab yaua walimu watatu Kenya

Muktasari:

  • Ni katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika Kaunti ya Garisa; walipua kituo cha polisi na kukata mawasiliano Kamuthe.

Garisa, Kenya. Kundi la wanamgambo wa Al Shabab limefanya mashambulizi matatu tofauti na kuua walimu watatu katika Kaunti ya Garissa, Kaskazini mwa Kenya.

Wanagambo hao pia wamechoma moto kituo cha polisi pamoja na kuharibu mfumo wa mawasiliano katika mnara uliopo eneo la Kamuthe.

Katika tukio la Garissa wanamgambo wa kundi hilo waliwapiga risasi hadi kufa walimu hao katika mji huo uliopo mpakani mwa Kenya na Somalia.

Taarifa ya Jeshi la Polisi nchini humo zilisema kuwa wanamgambo hao walitekeleza matukio hayo yote leo Jumatatu Januari 13.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kabla ya kufyatua risasi hizo wanamgambo hao waliweka vilipuzi chini ya ardhi katika maeneo mbalimbali.

Kenya imekuwa katika hali ya tahadhari baada ya kupata taarifa za kijasusi kwamba kundi la Al Shabab linapanga kufanya mashambulio zaidi.

Wiki iliyopita, Uingereza ilitoa onyo kwa raia wake wanaotaka kusafiri nchini humo dhidi ya kutembelea eneo hilo la Kaunti ya Garissa na katika eneo la ndani ya kilomita 60 katika mpaka wa Kenya na Somalia.

Hili ni shambulizi ya 11 kutekelezwa na kundi la Al Shabab nchini Kenya katika kipindi cha wiki sita. Mashambulizi manne yalitokea katika Kaunti ya Garissa, matatu eneo la Wajir huku Mandera na Lamu yakitokea.