Aliyekutwa akimfundisha mbwa kuendesha gari akamatwa

Los Angeles. Mkazi mmoja wa jimbo la Washington nchini Mrekani amekamatwa baada ya mfukuzano wa magari wa mwendo kasi ambao uliwaacha polisi wakiwa wamepigwa butwaa baada ya kumkuta mbwa wa mtu huyo akiwa nyuma ya usukani.

Tukio hilo lilitokea Jumapili jioni baada ya polisi kupigiwa simu kuhusu dereva mmoja kugonga magari mawili kusini mwa jiji la Seattle na kisha kukimbia, afisa wa polisi Heather Axtman aliliambia shirika la habari la AFP.

Aliongeza kwamba polisi walipata simu kadhaa kuhusu gari lilikokuwa liliendeshwa vibaya kwa mwendo wa zaidi ya kilomita 160 kwa saa.

Axtman alisema polisi walilifukuza gari hilo na walipolikaribia walishangaa kuona mbwa akiwa amekaa katika kiti cha dereva na mwanaume akiwa ameshika usukani huku akikanyaga mafuta na breki akiwa amekaa katika kiti cha abiria.

Mfukuzano huo ulimalizika baada ya polisi kuweka vyuma barabarani vilivyotoboa matairi ya gari hilo, na kumkamata Alberto Tito Alejandro, mwenye umri wa miaka 51, ambaye alitiwa mbaroni kwa makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuendesha gari huku akiwa ametumia dawa za kulevya.

"Mara baada ya kutiwa mbaroni, alikiri kwa maafisa wetu kwamba alikuwa akijaribu kumfundisha mbwa wake kuendesha gari," Axtman alisema.

"Nimekuwa askari kwa karibu miaka kumi, na nimeshuhudia madereva wengi wakijitetea baada ya kusimamishwa na polisi, lakini hii ni mara ya kwanza kwa mtuhumiwa kujitetea kwa kudai kwamba ni mbwa aliyekuwa anaendesha gari, aliongeza huku akicheka.