Aliyetoa taarifa za uongo kuwa ana corona nchini Tanzania akamatwa

Muktasari:

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Musa Kisinza (25) mkazi wa kijiji cha Mwakitolyo  wilayani Shinyanga kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kuwa ana maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Musa Kisinza (25) mkazi wa kijiji cha Mwakitolyo  wilayani Shinyanga kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kuwa ana maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Kisinza anadaiwa kumpigia simu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu akieleza kuwa ni mgonjwa wakati si kweli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,  Debora Magiligimba amesema baada ya kutoa taarifa hizo, timu ya madaktari inayotoa huduma eneo la halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini ilifika katika kijiji  hicho kumpatia huduma za awali lakini mtu huyo alizima simu na madaktari walishindwa kumpata jambo lililosababisha taharuki.

Kamanda Magiligimba amesema Aprili 15, 2020  saa 1 asubuhi kikosi kazi cha askari wa makosa ya kimtandao walifika eneo la Mwakitolyo namba 2 na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo .

Amesema mtuhumiwa huyo alikutwa akiendelea na shughuli zake katika machimbo na alipelekwa katika zahanati ya kijiji kufanyiwa vipimo vya awali vya magonjwa nyemelezi yanayoashiria kuwepo kwa uwezekano wa kuwa na corona lakini hakuwa na dalili za magonjwa hayo.

Amesema alipohojiwa alikiri kutoa taarifa hiyo na kwamba baadaye aliamua kuiharibu laini yake ya simu kwa kuivunja vunja na kuitupa.

Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi  kuacha masihara kuhusu corona, akisisitiza kuwa atakayetoa taarifa za uongo kuhusu ugonjwa huo atachukuliwa hatua kali.