Bashir huenda akanyongwa Sudan

Khartoum. Rais wa Sudan aliyetimuliwa madarakani Omar al Bashir anaweza kuhukumiwa kunyongwa kutokana na kuhusika katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1989 ambayo yalimueka madarakani na kuiangusha serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Sadiq al Mahdi.

Kwa sasa anashikiliwa kizuizini huku kesi yake ya kuuhujumu uchumi wa Sudan katika utawala wake wa miaka 30, ikiendelea kusikilizwa na mahakama mjini Khartoum.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, mwanasheria Mkuu wa Sudan Taj Al Sir Ali Al Habr amesema ameunda kamati kuchunguza mapinduzi ya kijeshi ya Juni 30, 1988 ambayo yaliongozwa na Bashir.

Matokeo ya uchunguzi huo yatakuwa msingi wa kuwashtaki wale wote waliohusika katika kukiuka mfumo wa kikatiba nchini Sudan wakati huo.

Iwapo watapatikana na hatia, waliohusika katika mapinduzi hayo ya kijeshi wanaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela au kunyongwa.

Hayo yanaripotiwa siku chache baada ya serikali ya mpito ya Sudan kupasisha rasmi sheria ya kuvunjilia mbali utawala wa rais aliyeondolewa madarakani wa nchi hiyo, Bashir na chama chake.

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok amesema kuwa, sheria ya kuvunjilia mbali utawala wa Bashir ilipasishwa katika kikao cha Baraza la Utawala wa Mpito na baraza la mawaziri.

Hayo yanajiri wakati ambao makundi ya kimataifa ya haki za binadamu, makundi ya waasi yaliyopigana dhidi ya vikosi vya Bashir kwa miaka kadhaa na wanaharakati mbalimbali wamekuwa wakisisitiza juu ya ulazima wa kiongozi huyo wa zamani kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Bashir anasakwa na ICC kwa uhalifu wa kivita huko Darfur.