Bomu laua watu wanne Somalia

Saturday January 18 2020

 

Mogadishu, Somalia. Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari likiwalenga wajenzi kutoka Uturuki limelipuka katika eneo la Afgoye, kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Mogadishu, Somalia limeua watu wanne, polisi wamesema.

Imeripotiwa kwamba gari hilo ambalo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi liligonga katika eneo ambapo makandarasi hao wa Uturuki pamoja na maafisa wa polisi walikuwa wakila chakula cha mchana, kulingana na ofisa wa polisi, Nur Ali ambaye alizungumza na Reuters kutoka Afgoye.

Haijulikani ni nani aliyetekeleza shambulio hilo lakini wakazi na maofisa wa polisi wanasema kwamba wapiganaji wa al Shabaab walijaribu kushambulia Afgoye, takriban kilomita 30 kutoka Mogadishu, jioni siku ya Ijumaa kabla ya kufukuzwa.

Kundi hilo linalohusishwa na wapiganaji wa al Qaeda limekiri kutekeleza mashambulio ya hapo awali katika kampeni zake za kuipindua serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

''Tulisikia mlipuko mkubwa na muda mfupi kukatokea moshi mkubwa hewani. Kabla ya mlipuko huo , wahandisi kadhaa wa Uturuki msafara wa magari wa polisi wa Somalia waliojihami walionekana katika eneo hilo,” kulingana na mfanyabiashara mmoja wa duka aliyezungumza na Reuters kutoka Afgoye.

Shirika la habari la Uturuki, Anadolu, limesema Waturuki wanne waajiriwa wa kampuni ya ujenzi wamejeruhiwa na wanapata matibabu hospitalini, limenukuu taarifa kutoka Ubalozi wa Uturuki mjini Mogadishu.

Advertisement

Desemba 28 takriban watu 73 walifariki kufuatia mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari wakati wa pilikapilika nyingi za asubuhi katika mji mkuu wa Mogadishu nchini Somalia.

Mlipuko huo ulitokea katika kituo kimoja cha kukagua magari katika eneo la makutano ya barabara mjini humo.

Advertisement