Breaking News

Boris: Wafungwa wa ugaidi hawapaswi kutolewa gerezani mapema

Sunday December 1 2019

London, Uingereza. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema watu waliotiwa hatiani kwa makosa ya ugaidi hawapaswi kuruhusiwa kutoka jela mapema.

Waziri Boris ametoa kauli hiyo siku moja baada ya mtu mmoja kuwashambulia kwa kisu na kuua watu wawili jijini London jana.

Boris alisema mwenyendo wa kuruhusu wahalifu katili kutolewa jela mapema umeonyesha kutofanya kazi nchini Uingereza.

“Ni lazima mamlaka husika zichukue hatua, hatuwezi kuruhusu wafungwa wa namna hii kuachiwa mapema ni hatari sana.”

Jumamosia iliyopita mwanaume huyo alitekeleza unyama huo muda mchache baada ya kutoka gerezani ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kifungo chake kumalizika.

Mshambuliaji huyo, Usman Khan aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela kutokana na makosa ya ugaidi aliua watu wawili na kujeruhi wengine watatu karibu na daraja mashahuri la mjini London.

Advertisement

Mkuu wa Polisi kitengo cha kupambana na  ugaidi mjini London, Neil Basu alisema mwanaume huyo alikuwa akihudhuria mafunzo ya kuwaelimisha wafungwa wakati alipofanya shambulio hilo.

Wakati huo huo, Malkia wa Uingereza, Elizabeth wa Pili ametuma salamu za rambirambi kufuatia mkasa wa vifo hivyo.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Malkia Elizabeth alisema kitendo hicho ni cha kikatili na hakipaswi kufumbiwa macho.

Katika hata nyingine, kiongozi wa chama cha upinzani cha Labor nchini Uingereza, Jeremy Corbyn amesema kuwa waliopatikana na hatia ya ugaidi sio lazima watumikie kifungo kikamilifu.

Corbyn alisema watu waliokutwa na hatia ya makosa ya ugaidi si lazima watumikie kifungo chao kikamilifu kwa sababu inategemea na mazingira yaliyosababisha kufungwa kwao.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Sky News, Corbyn ambaye ni mwanaharakati wa amani wa zamani alisema pia kuwa maafisa wa polisi hawakuwa na chaguo lingine ila kumpiga risasi mshambuliaji huyo.

Kiongozi huyo alisema anadhani hawakuwa na chaguo kwa sababu mtuhmiwa huyo alikuwa na dalili za kuwa na bomu alilokuwa amejifunga mwilini mwake.

Advertisement