Bunge Iraq laidhinisha kujiuzulu waziri mkuu

Monday December 2 2019

 

Baghdad, Iraq. Bunge nchini Iraq limeridhia hatua ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Adel Abdel-Mahdi.

Wiki iliyopita Waziri Mkuu, Mahdi alitangaza nia ya kujiuzulu baada ya wiki kadhaa za maandamano dhidi ya Serikali yake.

Hatua ya kuidhinisha kujiuzulu kwa waziri Mahdi ilifikiwa katika kikao cha dharura kilichokaa Jumapili Desemba Mosi. Hata hivyo, haijabainika mara moja ni nani atakayemrithi waziri huyo.

Akizungumza mara baada ya wabunge kupitisha hoja hiyo, Spika wa Bunge, Salim al Jabouri alisema Rais Barham Saleh anapaswa kumteua waziri mkuu mpya.

Kwa mujibu Katiba ya Iraq, Rais anatarajiwa kuwasilisha ombi la kumteua waziri mkuu mpya bungeni ili kuunda Serikali yake.

Waziri Mahdi alishika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, akiahidi mabadiliko makubwa kabla utawala wake kupingwa kwa maandamano makubwa yaliyodumu kwa siku sita na kusababisha watu 149 kuuawa.

Advertisement

Waandamanaji hao walikuwa wakishinikiza kufanywa kwa mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri, kupunguza mishahara ya maafisa wa juu na kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana jambo aliloahidi kulishughulikia.

Kwa mujibu wa waandamanaji hao, kiongozi huyo alishindwa kutimiza matakwa yao hivyo kurudi tena barabarani mwezi Oktoba.

Advertisement