Bunge labariki rais wa Misri aongoze hadi 2030

Muktasari:

  • Bunge la Misri lililosheheni wafuasi wa Rais Abdul Fattah al-Sisi limelaumiwa na upinzani kwa kutumiwa vibaya na Rais huyo kupitisha ajenda zake

Cairo,Misri.Bunge nchini Misri limeidhinisha marekebisho ya Katiba yatakayomwezesha Rais Abdul Fattah al-Sisi kuendelea kukaa madarakani hadi mwaka 2030.

Rais huyo anatarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2022 wakati muhula wake wa pili wa miaka minne utakapokamilika.

Lakini marekebisho hayo ambayo lazima yapigiwe kura ya maoni katika siku 30 zijazo, yatarefusha muhula wake wa sasa kwa miaka sita na kumruhusu kugombea tena urais mara nyingine tena.

Marekebisho hayo pia yatamwongezea  mamlaka zaidi dhidi ya idara ya Mahakama na vile vile kujumuisha majukumu ya kijeshi katika siasa.

Mwaka 2013,  Sisi aliongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais wa kwanza wa Misri aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohammed Morsi kufuatia maandamano ya kupinga utawala wake.

Sisi alichaguliwa mara ya kwanza kuwa Rais mwaka 2014 na alichaguliwa tena mwaka jana baada ya kupata asilimia 97 ya kura zilizopigwa.

Katika uchaguzi huo hakukabiliwa na ushindani mkali kwasababu baadhi ya washindani wake walijiondoa katika kinyang'anyiro cha kugombea urais na wengine kukamatwa.