Bunge labariki uchunguzi dhidi ya Trump

Friday November 1 2019

 

Washington. Bunge la Marekani limepiga kura kupitisha mchakato rasmi wa uchunguzi dhidi ya Rais Donald Trump, unaokusudia kumwondoa madarakani.

Azimio hilo limepitishwa Alhamisi kwa kura 232 dhidi ya 196, huku wabunge wote wa Republican wakilipinga, wakiungwa mkono na wabunge wawili wa chama cha upinzani cha Democratic.

Azimio hilo linafungua njia ya sheria za msingi za kumchunguza Rais lakini si kura ya kuamua iwapo wamchunguze rais au la.

Uchunguzi huo utaangalia iwapo Trump aliishinikiza Ukraine kumchunguza mpinzani wake kisiasa, Joe Biden pamoja na mtoto wake wa kiume Hunter.

Baada ya kura hiyo, Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa hiyo ''ni kampeni mbaya na kubwa dhidi yake katika historia ya Marekani.”

Kufuatia uamuzi huo, Ikulu ya Marekani imesema hatua ya Bunge kuidhinisha azimio la uchunguzi dhidi ya Rais Trump haikuzingatia haki na ni kinyume na Katiba.

Advertisement

Akizungumza muda mfupi baada ya azimio hilo, Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Stephanie Grisham amesema Trump hajafanya chochote kibaya na kwamba kitendo cha wanachama wa Democratic ni ukiukaji usiokubalika.

Kwa upande wake, meneja wa kampeni wa Trump, Brad Parscale amesema wapiga kura watawaadhibu wanachama wa Democratic wanaounga mkono suala hilo na kwamba kiongozi huyo wa Marekani atachaguliwa tena kwa urahisi.

Advertisement