China, Korea Kusini zinavyobeba matumaini ya dunia vita ya corona

Lipo swali; China na Korea Kusini zimewezaje? Ugonjwa ulianzia Jimbo la Wuhan, China, mapambano makali ya miezi mitatu yamebadilisha taswira yote.

China haijarekodi kifo kipya cha ugonjwa huo tangu Machi 12, mwaka huu.

Ni ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi vya SARS corona 2.

Yaani virusi vya corona vilivyosababisha homa ya mafua ya SARS iliyotikisa kati ya mwaka 2002 na 2004, nakala yake ya pili ndio inasababisha Covid-19. Janga la dunia kwa sasa.

Machi 12, mwaka huu, Kituo cha Mfumo wa Sayansi na Uhandisi Chuo Kikuu cha John Hopkins, Marekani, kilitoa taarifa kuwa watu 4,600 walikuwa wamefariki dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 duniani kote, kati ya hao, 3,304 pekee ni vifo vilivyotokea China ya nchi kavu.

Hesabu hiyo ilionyesha kati ya vifo vyote vya Covid-19, zaidi ya asilimia 65 ni vifo vilivyotokea China. Kutoka Machi 12 mpaka Machi 19 ni siku saba tu, taswira ikawa imebadilika. China ikapitwa idadi ya vifo na Italia.

Tangu Machi 12, China sio tu haijarekodi kifo kipya cha Covid-19, bali pia inaponyesha idadi ya wagonjwa kwa kasi kubwa. Kutoka makumi elfu ya waathirika, sasa China inatamba kuwa na wagonjwa wa Covid-19 wasiozidi 1,000. Na hilo ndilo swali, Wachina wamewezaje?

Ndio maana haishangazi kuona Rais wa Marekani, Donald Trump haiti tena SARS Corona 2 ni Chinese Virus (Virusi vya Kichina), kama alivyonukuliwa mara kwa mara, badala yake anampigia simu Rais Xi Jinping wa China, wanajadili jinsi ya kusaidiana kuutokomeza ugonjwa huo duniani.

Angalau siasa zinaondoka. Wachina wanapunguza matamshi yao kwamba SARS Corona 2 ni virusi vilivyotengenezwa na Wamarekani kama silaha ya kibaiolojia ili kuathiri uchumi wa China, kadhalika Trump haiti tena Chinese Virus. Ni janga la dunia.

Haishangazi kuona China inafunga mipaka ili kukwepa maambukizi kutoka nje. Covid-19 ilianza China, ikasambaa duniani kote na sasa ugonjwa umedhibitiwa ulipoanzia. Kwa sasa dunia ni hatari kwa China, kibao kimebadilika. Awali, China ndio ilikuwa hatari kwa dunia.

Na bila shaka, dunia sasa hivi inaitazama China kwa jicho la msaada wa matumaini. Kwamba maarifa yao ya kudhibiti Covid-19, yazifae na nchi nyingine. Dunia kiusalama, kidiplomasia na kiuchumi, itazidi kuwa taabani kama Covid-19 hautadhibitiwa.

Kama ambavyo China inatazamwa, ndivyo na Korea Kusini vivyo hivyo.

Dunia haijashuhudia taifa ambalo limepata asilimia kidogo ya vifo vya Covid-19 kama Korea Kusini. Tangu Januari 20, mwaka huu, mtu mmoja raia wa China mwenye umri wa miaka 35 aliyeingia Korea Kusini akitokea Wuhan, China, alipimwa na kugundulika ana maambukizi ya virusi vya corona, usambaaji wa maambukizi ni mdogo na vifo ni kidogo kuliko nchi yoyote ile ambayo Covid-19 imeshabisha hodi.

Mpaka Machi 29, mwaka huu, jumla ya watu 9,661 walibainika kuwa na maambukizi ya Covid-19, huku 5,228 wakitibiwa na kupona, vifo ni 158 tu. Idadi hiyo ya vifo ni sawa na asilimia 1.3 ya maambukizi yote.

Huo ni wastani mdogo ukilinganisha na asilimia 4.34 za vifo vilivyotokana na maambukizi ya virusi vya corona, kama zilivyokadiriwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Wakati jua la Machi 29, lilipochomoza, watu karibu 400,000 walikuwa wameshapimwa Korea Kusini. Wanaokutwa wameathirika wanatengwa ili kudhibiti maambukizi mapya. Upimaji wa Covid-19 unafanyika nchi nzima. Wastani wa watu 20,000 hupimwa kwa siku katika nchi hiyo.

Mtu unaweza kujiuliza, Korea Kusini wamewezaje?

Shirika la Habari la Al Jazeera, lilizungumza na Jerome Kim, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo (IVI) aliyesema vifo vya Covid-19 kwa Korea Kusini si vingi kwa sababu nchi hiyo imewekeza kwenye tasnia ya teknolojia ya kibailojia (robust biotech).

Kim anasema Korea Kusini ina kampuni nyingi za teknolojia ya biolojia, hivyo baada ya Covid-19 kugundulika, kampuni hizo zilitengeneza vifaa vingi vya upimaji vyenye kuwezesha watu 20,000 kupimwa kwa siku, kisha mpango wa upimaji kwa lazima ulianzishwa nchi nzima.

Ni kupitia mpango huo, imekuwa rahisi kuwabaini waathirika kabla hali haijawa mbaya na kuwapa huduma haraka.

Japokuwa tiba haijagundulika, angalau kwa utaalamu wa kutibu dalili hufanikisha watu wengi zaidi kupona, huku vifo vikiwa vichache kuliko nchi zote duniani.

Pia, maambukizi mapya yamekuwa yakidhibitiwa.

Piga hesabu kuwa Korea Kusini, ndani ya miezi miwili na siku 10, waathirika wa Covid-19 ni 9,661, wakati Italia ambayo ugonjwa ulifika Januari 31, mwaka huu, ndani ya mwezi mmoja na siku 29, waathirika walishafikia idadi ya watu 97,689.

Yupo mtu anaweza kudhani Italia ina msongamano mkubwa wa watu kulinganisha na Korea Kusini. Ndiyo maana maambukizi yamekuwa ya kasi na kushitua, vilevile idadi ya vifo ni kubwa kuliko sehemu yoyote ile.

Kwa mujibu wa sensa ya Umoja wa Ulaya ya mwaka 2018, Italia ilikuwa na watu milioni 60.5, wakati Korea Kusini ina watu milioni 51 4.

Eneo la Italia ni maili za mraba zaidi ya 300,000, Korea Kusini eneo lake ni maili za mraba 100,000. Hivyo, Korea Kusini kwa idadi ya watu na eneo lake, ina msongamano kuliko Italia.

Hiyo inamaanisha kuwa Korea Kusini ina maarifa makubwa ya kupambana na Covid-19, kuliko nchi yoyote ile duniani. Maarifa hayo wameyathibitisha kwa vitendo. Namba chache ya maambukizi, idadi kubwa ya wanaopona, namba chache ya vifo, kwa pamoja vinaipendelea Korea Kusini.

Kesi za waathithirika wa Covid-19 zilizofungwa Italia mpaka asubuhi ya Machi 30, mwaka huu ni 23,809. Watu 13,030 wamepona, wakati 10,779 ni vifo. Ni kuonyesha kuwa kesi zenye kufungwa Italia, asilimia 45 ni vifo, asilimia 55 wanapona. Na mpaka sasa, watu waliokufa Italia ni asilimia 11 ya maambukizi yote nchini humo.

Marekani inakabiliwa na maambukizi ya kishindo. Mtandao wa Worldometer ulionyesha Machi 30, mchana kuwa maambukizi yalifikia 143,025, vifo vikiwa 2,489, sawa na asilimia 1.7.

Huo ni wastani mkubwa mno wa maambukizi. Jumlisha vifo pia kama utalinganisha na Korea Kusini.

Baada ya takriban wiki mbili, Machi 29, mwaka huu, ndiyo China iliripoti maambukizi mapya 45, kati ya hao, waathirika 44 ni wageni waliopimwa na kugundulika na maambukizi baada ya kuingia. Hiyo ni kuonyesha kuwa China ilipata mgonjwa mpya mmoja katika wiki mbili.

Watu zaidi ya 75,576 wamepona China, vifo ni 3,304, na hakuna kifo ambacho kimeripotiwa tena.

Kwa sasa, watu 725,230 wameshathibitishwa kuugua Covid-19 duniani kote, wakati vifo ni 34,034. Tayari Covid-19 imeshafika kwenye nchi 177, sawa na asilimia 90.7 ya dunia.

Ni kipimo kuwa China na Korea Kusini zimebeba matumaini makubwa ya dunia, juu ya namna ya kulishinda janga la Covid-19.

Kwa namna yoyote, China na Korea Kusini zinapaswa kuchangia utaalamu wao ili kuisaidia dunia na kuifanya iwe huru dhidi ya Covid-19.