Corona ilivyobadili mtindo wa maisha China

Muktasari:

USULIVirusi vya corona viligunduliwa nchini China Desemba 30, mwaka 2019.Virusi vya aina hiyo kwa kawaida vinawaathiri wanyama lakini mara nyingine vinaweza kuwapata bin-adamu, kwa mfano mlipuko wa ugonjwa wa ‘Sars’ ambao uliuwa watu wengi China.Virusi vya corona vinamfanya mtu mwenye maambukizi kuwa na dalili za homa na kukohoa.

Miongoni mwa watu waliokufa kwa maambukizi ya virusi hivyo ni Daktari raia wa China, Li Wenliang aliyejaribu kutoa tahadhari kuhusu ugonjwa huo. Wenliang alipata maambukizi wakati akifanya kazi katika hospitali mjini Wuhan.Desemba 30, 2019 alituma ujumbe kwa madaktari wenzake akiwata-hadharisha kuvaa vifaa vya kujik-inga kuepuka maambukizi.

Daktari huyo aligundua visa saba vya maambukizi ya virusi ambavyo alifikiri kuwa vilifanana na Sars- mlipuko uliowahi kutokea mwaka 2003.Siku nne baadaye aliitwa na idara ya usalama ambapo aliamriwa kusaini barua. Katika barua hiyo alikuwa akishutumiwa ‘’kutoa taarifa za uongo’’ ambazo zilileta taharuki miongoni mwa jamii’’.Alikuwa mmoja kati ya watu wanane ambao polisi walisema walikuwa wakichunguzwa kwa makosa ya ‘’kueneza uzushi’. Hata hivyo baadae mamlaka zilimuomba radhi Dk Wenliang.

Kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi wa China kwa yamebadilika tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vipya vya corona.

Watu wamezuiwa kutoka katika makazi yao na shughuli nyingi za uzalishaji mali zimesimama. Huduma muhimu kama hospitali, magari ya usafi, maduka ya dawa na maduka ya kuuza vyakula ndizo zinazoendelea. Pia huduma za usafiri wa ndege kutoka na kwenda mji wa Wuhan, pamoja na usafiri wa treni, feri na mabasi nao umezuiwa.

Pamoja na hayo serikali imepiga marufuku ya muda uuzaji wa nyamapori katika masoko ya mji wa Wuhan ikihofia maambukizi mapya ya homa ya virusi hivyo.

Virusi hivyo vipya husababisha homa, ambayo dalili zake ni pamoja na mafua na kuongezeka joto la mwili na tayari zaidi ya watu 2,500 wameshapoteza maisha.

Tafiti za awali zinaonyesha kuwa virusi hivyo vimetokana na popo.

Tangu kuibuka kwa virusi hivyo, serikali ya China imetoa mazuio mbalimbali ili kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Mji wa Wuhan, ambako ndio chimbuko wa ugonjwa huo, na miji mingine 15 imewekwa karantini na watu takriban milioni 50 wamezuiwa kutoka nje.

Marufuku hiyo na nyingine zilizotolewa zimesababisha wananchi kubadili mtindo wa maisha na tofauti na siku nyingine, mitaa haina watu wengi.

Mfano, jiji la Beijing limekumbwa na ukimya kutokana na wakazi kutumia muda

mwingi wakiwa nyumbani.

“Sasa kuna watu wachache. Huwezi kwenda nje kwa ajili ya kufuata chochote, kukutana na marafiki au kula chakula cha jioni au cha mchana. Kila kitu kimesimamishwa,” alisema Yena Lei, mtaalamu wa fedha wa jijini Shanghai alipoongea na CNN.

Kwa kawaida jiji hilo ni tulivu, hasa wakati wa mwaka mpya wa jua wakati watu wanapochukua mapumziko ya muda mrefu kukaa na familia zao, lakini si kwa kiwango cha sasa.

Jijini Beijing, mitaa ni mitupu tofauti na hali yake ya kawaida katika mji huo mkuu wa China. Picha zinaonyesha watu wachache wakiwa mitaani tofauti na misongamano ya kawaida.

Na hata walio mitaani wanaoonekana wakiwa wamejifunika midomo na pua kwa kutumia maski, ili kujikinga na maambukizi yanayosambaa kwa hewa.

Pamoja na watu kuvaa vikinga mdomo na pua wanapotoka nje, pia wanapokutana husalimiana bila kushikana mikono.

Watu hao wanasema licha ya kutoshikana mikono, pia wamekuwa wakinawa mikono mara kwa mara ili kujihakikishia usalama dhidi ya ugonjwa huo.

Hata katika eneo la biashara ambako mara nyingi kunakuwa na umati mkubwa ya watu wakifanya huduma mbalimbali, sasa maeneo hayo yamekuwa kimya na wanaonekana watu wachache wakipita.

Pia kwenye usafiri wa treni za chini ya ardhi za Beijing ambako walikuwa wakihudumia wasafiri wengi, nako hali imekuwa tulivu. Wanaonekana watu wachache, hakuna shida ya kupata kiti cha kukaa.

Katika kuonyesha kuwa hali si nzuri nchini humo, watu wanalazimika kufanya mazoezi ndani ya vyumba kama shabiki wa riadha nchini humo, Pan Shancu alivyoeeza kuwa amekuwa akikimbia mbio za riadha ndani ya chumba chake.

Shancu aliliiambia AFP kwamba amekimbia kilomita 66 ndani ya chumba chake kwa kutumia saa 6 na dakika 41 kwa kuzunguka kitanda.

“Nilijisikia kizunguzungu mwanzo, lakini unazoea baada ya kuzunguka mara nyingi,” alisema Pan anayeonekana katika video inayosambaa nchini China. Pia alisema alikimbia kilomita 30 akiwa bafuni.

Ukiacha hayo, hivi sasa watu wanalazimika kupata huduma ya chakula na vinywaji wanavyopelekewa nyumbani kwa usafiri maalum baada ya kuagiza.

Pia wataalamu wamekuwa wakipita nyumba hadi nyumba kuangaalia afya pamoja na kuhakikisha kama kuna kisa kipya, huku mamlaka zikisisitiza kuwa kwa yeyote atakayebainika kuwa na dalili za awali aripotiwe kwa Serikali, ili apate huduma haraka katika vizuizi vyao na siyo kubaki nyumbani.

Kwa upande wa wanafunzi wanaosoma vyuo mbalimbali nchini huo, sasa wanalazimika kuendelea na masomo kwa njia ya mtandao wakiwa nyumbani.

Serikali ya China imewataka wanafunzi kufuata masharti, maelekezo na miongozo inayotolewa kwa ajili ya afya zao na ustawi kwa jumla.

Mmoja wa wanafunzi wanaosomea udaktari China, Majaliwa Bernard alisema changamoto waliyonayo ni upatikanaji wa chakula kwa sababu maeneo mengi yamefungwa na yale yaliyofunguliwa chakula kinauzwa kwa bei ya juu.

Pia alisema changamoto nyingine ni upatikanaji wa maski.

Pamoja na juhudi hizo, mpaka sasa ugonjwa huo ulioibuka mwishoni mwa mwaka jana nchini humo umeshaua zaidi ya watu 2,500 nchini humo.

Kwa mujibu wa takwimu hadi sasa watu wasiopungua 79,000 wameambukizwa virusi hivyo duniani, huku China wakiwamo watu wasiopungua 18,000 waliopata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitali.

Ugonjwa huo ambao umeshatangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni janga la dharura, umeshaenea katika nchi zaidi ya 30 ikiwamo Iran, Marekani, Uingereza, Australia, Italia, Thailand, Korea Kusini, Japan, Canada, Ufaransa, Umoja wa Falme za Kiarabu au Imarati.

Msemaji wa WHO, Christian Lindmeier alikaririwa na mtandao wa Sauti ya Amerika (Voa) akisema kufunga mipaka hakuwezi kuzuia kirusi hicho.

“Kama sote tunavyojua katika matukio mengine ya maambukizi, iwe Ebola au magonjwa mengine, pale watu wanapotaka kusafiri, watafanya hivyo. Na iwapo njia rasmi za kupita zikiwa zitafungwa, watapita katika njia za panya,” alikaririwa Lindmeier.

“Lakini njia pekee ya kudhibiti maambukizi ni kupima iwapo mtu ana homa, kwa mfano, kutambua historia ya safari yake, kujaribu kufuatilia nani anapita katika mpaka wako na kuona iwapo wana dalili zozote za maambukizo ni kupitia mipaka rasmi.”

Alisema nchi zina haki ya kiutawala kuchukua hatua zozote wanazoamini ni bora katika kuwalinda raia wao na wanataraji katazo la kusafiri litakuwa la muda mfupi, ili watu waendelee na maisha yao.