Corona yaingia Afrika

Muktasari:

Kisa cha kwanza cha virusi vya corona kimethibitishwa barani Afrika katika nchi ya Misri

Cairo, Misri. Hatimaye virusi vya ugonjwa wa corona (covic-19) vimethibitishwa kuingia barani Afrika.

Wizara ya Afya ya Misri, imethibitisha kutokea kwa mgonjwa wa kwanza katika nchi hiyo.  

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo leo Jumamosi Februari 15, ilisema mgonjwa aliyebainika siyo raia wa Misri ingawa mpaka sasa hakufahamika ni wan chi gani.

Kwa mujibu taarifa hiyo, maafisa wa afya wa Misri waligundua mgonjwa huyo kupitia mpango wa kuwafuatilia abiria waliowasili kutoka nchini ambazo zina virusi vya corona.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Misri, Khaled Megahed alisema serikali inafuatilia kwa karibu afya ya mgonjwa huyo ambayo imeripotiwa kuwa imara.

Mamlaka za Misri pia zimeliarifu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusiana na kisa hicho na tangu wakati huo mgonjwa huyo amewekwa karantini.

Mapema mwezi huu Misri ilifuta safari zote za shirika la ndege ya taifa kwenda China. Aidha, serikali ya nchi hiyo iliwaondoa raia wake 301 waliokuwa katika mji wa Wuhan ambao ni kitovu cha mlipuko huo wa virusi hivyo ambako baada ya kuwasiliwa waliwekwa karantini kwa siku 14.