Corona yatangazwa kuwa janga la kimataifa

Muktasari:

Uamuzi huo umetangazwa jana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Geneva, Uswizi.  Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza mlipuko wa virusi vya corona kuwa ni janga la kimataifa.

Tangazo hilo limekuja wakati ambako zaidi ya nchi 80 zimeshakumbwa na maambukizi ya virusi hivyo ambavyo vilianza katika mji wa Wuhan, China miezi mitatu iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika hilo hilo mpaka sasa zaidi ya watu 100,000 wameambukizwa virusi hivyo huku 4,600 kati yao wakifariki dunia.

Mkurugenzi Mkuu WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema jana kuwa idadi ya visa nje ya China vimeongezeka mara 13 katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita.

Kiongozi huyo alisema anahofu kubwa kutokana na viwango vya maambukizi ya virusi vinavyoendelea kwa kasi duniani kote.

Mwezi uliyopita shirika hilo lilikataa kutangaza virusi hivyo kama janga la kitaifa kwa madai kuwa havifikia viwango vya kutangazwa hivyo.

Hata hivyo, Dk Tedros alisema kuuita ugonjwa huo janga haimaanishi kuwa WHO inabadilisha ushauri wake juu ya kile mataifa yanapaswa kufanya.

Mkurugenzi huyo alizitaka serikali mbalimbali duniani kubadili jinsi njia za kushughulikiwa mlipuko huo na kuchukua hatua za dharura.

“Nchi kadhaa zimeonyesha kuwa virusi hivi vinaweza kudhibitiwa iwapo kutakuwa na njia madhubuti,”

Alisema kinachotakiwa sasa ni kuweka uwiano unaofaa kati ya kulinda afya, kupunguza maambukizi haki ya maisha ya binadamu.