Virusi vya corona, vyaua 242 kwa siku moja

Thursday February 13 2020

 

Wuhan, China. Watu 242 wamepoteza maisha kwa siku moja katika Jimbo la Hubei, China kutokana na virusi vya corona (covid-19).

Vifo hivyo vimesababisha idadi ya waliokufa mpaka leo Alhamisi Februari 13, kufikia 1,310 tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi hivyo miezi mitatu iliyopita nchini China.

Shirika la habari la AFP lilisema vifo hivyo vipya ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya kila siku vinavyotokea katika jimbo hilo. Jumatatu iliyopita watu 103 walifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Tume ya Afya nchini China ilisema idadi ya maambukizi mapya katika jimbo la Hubei ambalo ndiyo kitovu cha virusi hivyo imefikia watu 14,840 kwa siku.

Tume hiyo ilisema idadi hiyo imeanza kuwajumuisha watu ambao wanachunguzwa kupitia mbinu mpya za kitabibu kuanzia leo.

Kwa mujibu wa tume hiyo, lengo ka kujumuisha watu hao ni baada ya mapitio kuhusu data zake za nyuma na kushuku maambukizi.

Advertisement

Vyombo vya habari vya serikali nchini China vilisema wiki iliyopita kuwa Hubei itaanza kutambua matokeo ya uchunguzi wa kompyuta CT scan ili kuthibitisha maambukizi na kuruhusu hospitali kuwatenga wagonjwa kwa haraka zaidi.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn ameutaka Umoja wa Ulaya (EU), kuwajibika kuhusu maambukizi ya virusi vya corona kwa kutenga fedha zaidi ili kudhibiti ugonjw ahuo.

Waziri Spahn anatarajia kukutana na mawaziri wa afya wa Umoja huo mjini Brussels leo kujadili kuhusu ugonjwa huo.

“Ombi la msaada wa fedha la Shirika la Afya Duniani (WHO) lisijibiwe tu na nchi badala yake EU ichukue juhumu,” alisema.

Spahn alisema ana matumaini mataifa wanachama wa EU yatakubaliana kuchukua hatua katika uratibu ili kupunguza maambukizi ya virusi hivyo.

Awali Kamishna wa Afya wa EU, Stella Kyriakides alisema Umoja huo unahitaji kuchukua hatua kwa changamoto hiyo kwa kuwa virusi havijali mipaka.

Advertisement