Dunia yazungumzia kifo cha kiongozi wa kundi la Dola ya Kiislamu Abu Bakr al-Baghdadi

"Yuko wapi Baghdadi wetu,” ilikuwa kauli ya Rais Donald Trump wakati akitangaza kuthibitisha kifo cha kiongozi wa kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu (IS) huku viongozi mbalimbali wa dunia wakitoa maoni yao.

Licha ya Rais Trump kuzishukuru nchi za Urusi, Uturuki, Syria, Iraq na kikundi cha wapiganaji wa kundi la Kurd wa Syria kwa kufanikisha kumuangamiza kiongozi wa IS, Abu Bakr al-Baghadadi, baadhi ya viongozi wameibeza.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alituma ujumbe kwenye twitter akisema mauaji ya al-Baghdadi ni jambo muhimu katika vita dhidi ya ugaidi.

Amesema tukio hilo ni kielelezo muhimu kuhusu vita ya pamoja ya ugaidi na kwamba Uturuki itaendelea kuunga mkono juhudi za kupambana na ugaidi.

Russia

Waziri wa Ulinzi wa Urusi kwenye ujumbe wake wa twitter alishuku taarifa hiyo ya Rais Trump, akisema hawakuwa na habari za uhakika kuhusu operesheni ya Marekani.

“Wizara ya Ulinzi ya Urusi haikuwa na taarifa za uhakika kuhusu kilichokuwa kinafanywa askari wa Marekani kwenye eneo la mapigano la Idlib lililopo mpaka wa Uturuki,” amesema Meja Jenerali Igor Konashenkov wa Urusi.

Afghanistan

Serikali ya Afghanistan imeunga mkono juhudi zilizofanywa na majeshi ya Marekani hadi kufanikisha kifo cha kiongozi wa IS, Abu Bakr al-Baghadadi.

Msemaji wa Serikali ya Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani alituma twitter yenye ujumbe uliosema nchi hiyo inaungana na Marekani.

Israeli

Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu amelielezea tukio kuwa ni ‘mafanikio yenye kuvutia.’

“Hii inaonyesha matamanio yetu, ya Marekani na ya nchi zote zilizo huru katika kupambana na vikundi vya kigaidi yakiwamo mataifa yanayounga mkono magaidi,” amesema Netanyahu.

Netanyahu ameongeza kuwa; “Mafanikio haya ni muhimu, lakini mapambano bado yanaendelea.”

Iran

Waziri wa Habari wa Iran, Mohammed Javad Azari-Jahromi amesema kwenye ujumbe wake wa twitter kuwa kifo cha al Baghdadi siyo jambo kubwa ni kama vile wamekiua kitu walichokiunda wenyewe. Hata hivyo, Jazad hakufafanua kauli yake hiyo, Iran mara kadhaa bila kuonyesha ushahidi imekuwa ikiishutumu Marekani kuunda kundi hilo la kikaidi.

Bahrain

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain, Khalid bin Ahmed Al Khalifa alipongeza Marekani kwamba kilichotokea ni janga kubwa kwa kundi hilo la kigaidi.

Ufaransa

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly alitahadharisha kwamba vita dhidi ya kundi hilo bado inaendelea.

Amesema Ufaransa itaendelea na mapambano vita dhidi ya ugaidi bila kupumzika, kwa kushirikiana na washirika wao.

Uingereza

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema ni taarifa muhimu lakini ameonya kwamba vita dhidi ya kundi hilo bado haijamalizika.

Boris amesema kifo cha al-Baghdadi ni habari nzuri katika vita dhidi ya ugaidi, lakini mapambano dhidi ya waovu bado ianendelea.

Amesema wataendelea kushirikiana katika mapambano dhidi ya vikundi vya ugaidi hadi watakapowaangamiza wote.