EU yakataa madai ya Boris kuhusu Brexit

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa EU, kiongozi huyo wa Uingereza mpaka sasa hajatoa mbadala unaoweza kufanyakazi.

London, Uingereza. Umoja wa Ulaya (EU) umekataa madai ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kuondoa mpango wa kutokuwa na ukaguzi mpakani ili kufikia makubaliano ya Brexit.

Kwa mujibu wa EU, kiongozi huyo wa Uingereza mpaka sasa hajatoa mbadala unaoweza kufanyakazi.

Jumanne iliyopita, Boris alimwandikia Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk akisisitiza kwamba Uingereza haiwezi kukubali kile inachoita hatua ya kutokuwa na ukaguzi mpakani ambayo ni kinyume na demokrasia, utaratibu ambao utaweza kuepukwa kati ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja huo na Ireland ya kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza.

Tangu alipoingia madarakani mwezi uliopita, Boris amekuwa akisisitiza kwamba Uingereza itajitoa kutoka Umoja huo ifikapo Oktoba 31.

Kwa sasa waziri mkuu huyo ameongeza kasi ya matayarisho kwa ajili ya kujitoa bila makubaliano hali ambayo inaelezwa kwamba inasababisha mvurugiko mkubwa wa kiuchumi.