Hasimu wa Netanyahu ashindwa kuunda serikali Israel

Mkwamo umeendelea nchini Israel baada ya kiongozi wa upinzani, Benny Gantz pia kushindwa kuunda serikali na hivyo kupisha njia ya kufanyika uchaguzi wa tatu ndani ya mwaka mmoja.

Israel imekwishafanya uchaguzi mara mbili, mwezi Aprili na baadaye Septemba lakini mara zote imeshindwa kuunda serikali kwa kuwa hakukuwa na mshindi aliyepata idadi ya viti 61 vinavyotakiwa.

Kiongozi wa chama cha Blue and White, Benny Gantz  amenyoosha mikono katika suala kuunda serikali ambalo pia lilishamshinda mpinzani wake, Waziri mkuu Benjamin Netanyahu na kuibua uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa tatu.

Kiongozi huyo alikuwa na muda wa siku 28 wa kuunda serikali baada ya Netanyahu wa chama cha Likud kushindwa kuiunda serikali.

Rais wa Israel Reuvin Rivlin anatarajiwa kuliarifu Bunge na kulikabidhi mamlaka, hatua itakayofungua milango chombo hicho kutafuta mbunge yeyote katika Bunge hilo lenye jumla ya viti 120, kutafuta uungwaji mkono, ili kuunda serikali, ikiwa ni mara ya kwanza kwa taifa hilo la Israel.

Ikiwa hilo litatokea, Sauti ya Ujerumani (DW) inaripoti kuwa, mbunge atakayeteuliwa pamoja na Gantz na Netanyahu, watapewa siku 2, kutafuta uungwaji mkono wa wabunge 61 na kujaribu kuunda serikali ya muungano.

Mbunge atakayepata uungwaji mkono kama huo, atapewa muda wa siku 14 kuunda serikali.

Ikiwa na hilo litashindikana, utaitishwa uchaguzi mpya ambao huenda ukafanyika Machi mwakani. Gantz amemshukuru Rais Rivlin kwa kumuunga mkono na kusema kwamba ataendelea na juhudi za kuunda serikali kwa ajili ya watu wa Israel.

"Hizi ni siku 21 za mwisho ambapo demokrasia ya Israel itakuwa katika mtihani mkubwa. Hata wakati huu nitajitokeza na kutumia rasilimali zote ili mazungumzo yafanyike haraka na kutoa taswira ya matokeo ya uchaguzi na kuunda serikali itakayoiondoa Israel katika mkwamo uliosababishwa na watu walioweka vihunzi," alisema Gantz. 

Netanyahu ameeleza utayari wake wa kurejea katika majadiliano ya kuunda serikali baada ya jaribio la Gantz kushindwa.

Uamuzi wa kiongozi huyo wa Blue and White ulikuja saa chache baada ya muda wa mwisho aliopewa kumalizika Jumatano usiku.

Gantz alikwama kutokana na uamuzi wa mwanasiasa Avigdor Lieberman wa chama cha mrengo wa kulia cha Yisrael Beiteinu, kukataa dakika za mwisho kuwaunga mkono Netanyahu na Gantz kushika cheo cha waziri wakuu, akisema wote wawili ni wa kushutumiwa kwa kushindwa kuunda serikali.

Tangazo lake lilikuwa ni ishara nyingine ya Israel kuelekea katika uchaguzi. Lieberman ana viti nane bungeni na hivyo kushikilia uzani wa madaraka baina ya Gantz na Netanyahu.

Katika uchaguzi wa Septemba chama cha Gantz kilipata viti 33 sawa na asilimia 25.95 wakati Likud ya Netanyahu ilipata viti 32 sawa na asilimia 25.1.