Hivi ndivyo wagonjwa wanavyosaidiwa wakiwekwa karantini ya corona

Dar es Salaam. Ofisa programu wa elimu ya afya kwa umma nchini Tanzania, Dk Tumaini Haonga amesema wagonjwa wanaotengwa karantini hawapewi dawa za moja kwa moja za kutibu corona kutokana na ugonjwa huo kutokuwa na tiba badala yake wanapewa dawa zinazotibu dalili au madhara ya yaliosababishwa na ugonjwa huo.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Machi 31, 2020 alipoulizwa huwa wagonjwa wanapiokuwa karantini wanafanya nini Dk Haonga amesema, “Wagonjwa wanapowekwa karantini kule wanapewa tiba za kutibu dalili au madhara yanayoletwa na hiki kirusi mwilini, kwa kutibu dalili na madhara tayari unaupa mwili nguvu ya kuweza kupambana na hatimaye mwili unafanikiwa kuviondoa kabisa virusi hivyo, vinakufa na vinamezwa kabisa na seli za mwili,"amesema
“Kama mgonjwa anatapika atapewa dawa za kuzuia kutapika, kama anaumwa kichwa atapewa dawa za kutuliza maumivu lakini kama ameshindwa kupumua atawekewa mashine za kumsaidia kupumua, hicho ndicho kinachofanyika,” amesema.
Pia, amebainisha kuwa kitu kingine wanachopewa wagonjwa ni lishe bora ili kinga za mwili ziweze kupambana na kirusi hicho
“Wanapewa chakula ambacho ni mlo kamili ambacho ni eneo muhimu sana katika kufanya kinga ya mwili isishuke, huu ugonjwa kitakachompa mtu nafuu ni kinga ya mwili, mwenye kinga imara ana uwezo mkubwa wa kupambana na kupona,"amebainisha
Mtaalam huyo amesema kuwa kitu kingine wanachopewa wagonjwa waliotengwa karantini ni ushauri wa kisaikolojia ili mwili usidhoofike “Vilevile wanapewa unasihi wa kisaikolojia na akili inakuwa saawa na mwili haudhoofu."
Dk Haonga ametoa rai kwa jamii isitumie dawa yoyote wanapojihisi wanaumwa kabla ya kupata vipimo na ushauri kutoka kwa wataalum
“Sio kwamba kuna dawa maalumu wanazopewa wagonjwa wa corona, mtu gani apewe nini inatokana na dalili alizonazo mgonjwa, hivyo hatuwezi kusema wanavyopewa wagonjwa karantini vinaweza kufanyika kweneye jamii bila watalam wa tiba.”
Amesema kwa sasa muitikio kwa jamii wa namna ya kujikinga na maambukizi hayo ni mkubwa japokuwa ni maisha mapya katika jamii
“Muitikio ni mkubwa sana, hata ukitembea kwenye mitaa unaona watu wameweka sehemu za kunawia mikono, tunahitaji kuweka nguvu zaidi kwa sababu huu ni mfumo ambao ni mpya watu hawakuuzoea”
“Kikubwa tunachofanya ni kuwasisitiza wananchi kufuata masharti ili kwa kuwa ugonjwa upo nchini usije ukasambaa zaidi” amesisitiza Dk Haonga.