Idadi ya waliokufa kutokana na kimbunga Japan yafikia 66

Muktasari:

Jumapili iliyopita Kimbunga Hagibis kiliipiga Japan na kusababisha madhara makubwa nchini humo.

Japan. Idadi ya watu waliokufa kutokana na Kimbunga Hagibis kilichotokea nchini Japan mwishoni mwa wiki imefikia 66.
Jumapili iliyopita Kimbunga Hagibis kiliipiga Japan na kusababisha madhara makubwa nchini humo.
Inaelezwa kuwa kimbunga hicho ni kikubwa zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 60 iliyopita ambako kimesababisha maporomoko ya ardhi.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilianza  kunyesha kuanzia usiku wa kuamikia Jumapili katika Peninsula ya Izu, Kusini Magharibi mwa Tokyo na kuendelea kupanda katika pwani ya Mashariki na kasi ya upepo ya kilometa 225 kwa saa.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Ufaransa (AFP), watu 56 wamefariki dunia kutokana na upepo mkali kusomba magari na kubomoa nyumba.
Kimbunga hicho pia kilisababisha mechi mbili za Kombe la dunia la mpira wa miguu na Rugby kufutwa. Shirika la Hali ya hewa la Japan (JMA) lilisema vipimo vinaonyesha kuna mvua kubwa ambayo haijawahi kutokea inatanyesha nchini humo huku waziri mkuu akisema Serikali itafanya kila iwezalo na kuongeza idadi ya askari na vikosi vya dharura.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Al Jazeera, juhudi za uokozi zinaendelea wakati Taifa hilo likijaribu kukabiliana na maafa yaliyotokea.
limeripoti kuwa karibu nusu ya vifo 66 vimetokea Kaskazini Mashariki ya maeneo ya Miyagi na Fukushima ambayo yalikumbwa na tetemeko la ardhi, Tsunami na kuharibika kwa kinu cha nyuklia mwaka 2011.
Hata hivyo, shughuli za uokozi bado zinakabiliwa na changamoto kufuatia kupasuka kwa kingo za mito 47 na kimbunga hicho kuleta maporomoko ya udongo na tope yaliyokatiza usafiri wa barabara.