Iran ‘yaigomea’ Marekani

Muktasari:

  • Yakataa mazungumzo baina yake na Marekani kuhusu mzozo wa mafuta.

Tehran, Iran. Kiongozi Mkuu wa Kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei amesema hakutakuwa na mazungumzo ya ngazi yoyote na Marekani.
Kauli hiyo sasa inamaanisha kwamba dhana ya uwezekano wa kufanyika mkutano kati ya marais wa mataifa hayo mawili baadae mwezi huu imekufa.
Televisheni ya Taifa ya Iran, imemnukuu waziri Khamenei akisema kuwa huo ndio msimamo wa uongozi mzima wa nchi yake na maafisa wote katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Awali kulikuwa na taarifa zenye kueleza uwezekano wa kufanyika kwa mkutano kati ya Rais Donald Trump na mwenziwe wa Iran, Hassan Rouhani, wakati wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa inayotarajiwa kufanyika mwezi huu mjini New York, Marekani.
Hata hivyo, Iran mara zote imeitaka Marekani kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.
Tangazo la Iran limekuja wakati Jumatatu iliyopita Trump alitangaza kwamba inaonyesha kama Iran ilikuwa nyuma ya shambulio la bomu dhidi ya eneo la viwanda vya mafuta vya Saudi Arabia.
Katika hatua nyingine, wakati bei ya mafuta ikipanda, Rais Donald Trump ametuma ujumbe kwamba nchi yake inaweza kutumia mafuta waliyonayo  kuhakikisha usambazaji upo sawa katika masoko.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, nchi hiyo ina takriban mitungi milioni 640 iliyowekwa katika mapango yaliyofichwa nchini humo.
Hatua hiyo inafuatia mashambulio katika vituo vikuu  viwili vya mafuta Saudi Arabia yaliyofanywa hivi karibuni na kuhusisha ndege 10 zisizo na rubani.