Iran yakiri kutungua ndege ya Ukraine

Tehran. Hatimaye Serikali ya Iran imekiri kuitungua ‘kwa bahati’ mbaya ndege ya Ukraine iliyoua watu 176, ikisema ni “kosa lisilosameheka.”

Ndege ya Ukraine aina ya Boeing 737-800 ilianguka Jumatano asubuhi muda mfupi baada ya kuruka wakati Iran ikirusha makombora dhidi ya kituo cha kijeshi cha Marekani nchini Iraq kulipiza kisasi kwa mauaji ya kiongozi wake wa kijeshi, Qasem Soleimani.

Taifa hilo limeeleza kujutia kitendo hicho kilichosababisha maafa makubwa, amesema Rais wa Iran Hassan Rouhani kupitia ukurasa wake wa Twitter.

“Uchunguzi wa ndani wa vyombo vya dola umebainisha kuwa kwa bahati mbaya makombora yaliyorushwa kwa makosa ya binadamu yalisababisha ndege ya Ukraine kuanguka na vifo vya watu 176 wasio na hatia,” aliongeza.

“Uchunguzi unaendelea kuwatambua na kuchukua hatua kwa kosa hilo lisilokuwa na msamaha.”

Mapema,  Shirika rasmi la habari la Iran, IRNA lilichapisha taarifa ya Jeshi la nchi hiyo ikisema Boeing 737 ilidhani ni ndege ya adui katika kipindi ambacho vitisho vya adui vilikuwa katika kiwango cha juu.

Taarifa za kukiri kosa hilo zimekuja siku moja baada ya Mamlaka ya Anga ya Iran kukanusha madai kuwa ndege hiyo ilitunguliwa, huku shinikizo la kimataifa likiongezeka kuitaka Iran ifanye uchunguzi unaoaminika baada ya nchi kadhaa za magharibi kusema ilitunguliwa.

Abiria wengi katika ndege hiyo walikuwa raia wa Iran waliokuwa 82 ikifuatiwa na Canada (63), Ukraine 11, Sweden 10, Afganistan 4 pamoja na Uingereza na Ujerumani zilizokuwa na abiria watatu kila moja..