Iran yashambulia kambi za Marekani zilizoko Iraq

Muktasari:

  • Wakati uhasama kati ya Marekani na Iran ukizidi kupamba moto, Iran imeshambulia kambi mbili za kijeshi zinazotumiwa na vikosi vya Marekani pamoja na vikosi kutoka mataifa mengine ikiwa ni njia ya kulipiza kisasi baada ya kuuawa kwa kamanda wa jeshi la Iran, Qassem Soleimani wiki iliyopita.

Tehran. Iran imeshambulia kwa makombora kadhaa kambi mbili tofauti zinazotumiwa na vikosi vya Marekani nchini Iraq, jeshi la Marekani limethibitisha.

Makombora hayo yalishambulia kambi ya Ain-Asad iliyopo katika jimbo la Anbar na kambi nyingine ya Erbil leo Januari 8, jambo ambalo limeongeza uhasama kati ya Marekani na Iran baada ya vikosi vya Marekani kumuua kamanda wa jeshi la Iran, Qassem Soleimani.

Iran imeapa kulipiza kisasi baada ya kuuawa kwa watu wake muhimu na shambulizi hili linachukuliwa kama kisasi cha Iran kwa Marekani kama walivyoahidi viongozi wake mara kadhaa wakati wa msiba wa Soleimani.

Katika taarifa yake, jeshi la Iraq limethibitisha kutokea kwa mashambulizi 22 katika kambi zilizopo Anbar na Erbil nchini humo.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba makombora 17 yaliilenga kambi ya Ain al-Asad wakati makombora matano yakielekezwa katika kambi ya Erbil ambayo ni kambi ya muungano wa majeshi kutoka nchi mbalimbali.

Hata hivyo, w3amedai kwamba hakuna kifo wala majeruhi kwa upande wa vikosi vya jeshi la Iraq.

Norway nayo imetoa taarifa kwamba hakuna askari wake hata mmoja aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulizi hilo lililotekelezwa na Iran, msemaji wa jeshi la Norway, Brynjar Stordal alinukuliwa na shirika la habari la Reuters. Amesema nchi yake ina askari 70 nchini Iraq.

Kwa upande wao, jeshi la Denmark nalo limesema hakuna askari wake waliopoteza maisha wala kujeruhiwa katika shambulizi hilo katika kambi ya Al-Asad.

Denmark ina askari 130 katika kambi hiyo ambayo imeunganisha askari kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kupambana na kikundi cha magaidi cha Islamic State (Isis).

Hata hivyo, kituo cha televisheni ya Taifa cha Iran kimetangaza kwamba takribani askari 80 wa jeshi la Marekani wamekufa katika shambulizi hilo.

Kituo hicho cha televisheni kikimnukuu ofisa mmoja wa jeshi kimeripoti kwamba Iran imeyalenga maeneo mengine 100 katika ukanda huo endapo Marekani itaamua kulipiza kisasi.

Pia, kituo hicho kimeripoti kwamba helikopta za Marekani pamoja na vifaa vingine vya kijeshi vimeharibiwa vibaya kwenye shambulizi hilo lililofanyika usiku wa kuamkia leo.

Wakati hayo yakijiri, India na Pakistan zimetoa tahadhari kwa wananchi wao wanapanga kwenda Iraq kuchukua tahadhari kwa sababu ya mashambulizi hayo yanayoendelea nchini humo. Wananchi wa mataifa hayo waliopo Iraq wametakiwa kuwasiliana na balozi zao kwa karibu zaidi.