Iraq yatangaza neema kwa wananchi kumaliza maandamano Iraq

Monday October 7 2019

Baghdad, Iraq. Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdel-Mahdi ametangaza hatua kadhaa za mageuzi na msaada wa kijamii akilenga kumaliza maandamano makubwa ya umma dhidi ya Serikali.

Mageuzi yao yanajumuisha kuwatambua wale waliouawa wakati wa maandamano kuwa mashujaa na wote waliojeruhiwa watapatiwa matibabu kwa gharama za Serikali ikiwamo kuwasafirisha kwenda nje.

Hatua hiyo inafuatia zaidi ya watu 100 kupopoteza maisha nchini humo baada ya waandamanaji wanaopinga Serikali kukabiliana na polisi.

Kwa mujbu wa Shirika la habari la AFP, vifo hivyo vimetokana na makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama ambako ainadaiwa kuwa polisi walitumia risasi za moto.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Oktoba 7, Waziri Mkuu Abdel-Mahdi alisema Serikali pia itazindua mpango wa kujenga makazi 100,000 kote nchini Iraq.

“Kipaumbele ni kujenga katika majimbo yaliyo masikini zaidi,” alisisitiza waziri mkuu huyo.

Advertisement

Aidha, waziri mkuu Abdel-Mahdi alisema pia Serikali yake itagharamia mafunzo ya kazi kwa raia 150,000 wasio na ajira na kisha kuwapatia mikopo nafuu ya kuanzisha biashara ndogo na za kati.

Hali ya utulivu imerejea mjini Baghdad huku ulinzi ukiwa umeimarishwa baada ya siku tano za maandamano dhidi ya Serikali yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 100.

Advertisement