Italia sasa hakuna kutoka nje kuzuia maambukizi zaidi ya corona

Sunday March 22 2020

 

Roma. Wakati idadi ya waliokufa kwa ugonjwa wa corona nchini Italia wakifikia 4,825 hadi leo asubuhi Jumapili Machi 22, 2020, Serikali  imeimarisha zuio la watu kutoka nje ili kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa huo.

Katika jitihada zake za hivi karibuni za kukabiliana na virusi vya corona vinavyosambaa na kuwaambukiza watu kwa haraka nchini humo, Italia imeamua kufunga karibu biashara zote hadi Aprili 3, 2020 isipokuwa zile za muhimu zinazohusika na ugavi wa mahitaji muhimu nchini kote.

Kwa mujibu wa shirika la habari la DW, Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte amesema huduma hizo ni  maduka ya vyakula, dawa na huduma ya posta. Amesema huduma hizo zitaendelea kufanya kazi kwa ajili ya kukimu mahitaji ya watu ya kila siku.

Mpaka jana Jumamosi, idadi ya maambukizi ilifikia 304,500 ulimwenguni kote wakati idadi ya vifo ikifikia 13,000.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kwamba watu 94,625 waliokuwa wameambukizwa ugonjwa huo wamepona.

Takriban watu bilioni moja ulimwenguni kote wamebaki majumbani wakati ambapo nchi kadhaa zimeweka amri ya kutotembea bila ya kuwa na sababu maalum ikiwa ni harakati za kuzuia kuenea kwa maambukizi.

Advertisement

Mkurugenzi wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema anaamini njia ilizotumia China kukabiliana na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona zinaweza kutoa mwanga wa matumaini katika kupambana na janga hili ijapokuwa wapo wanaohoji ikiwa mkakati wa China unaweza kufuatwa na nchi zingine.

Viongozi wa kidini wanaunga mkono hatua za watu kubakia majumbani mwao ili kuepusha mikusanyiko mikubwa ya watu ambapo hatari ya maambukizi inaweza kuwa kubwa.

Tangu Alhamisi iliyopita, Italia ilichukua nafasi ya kwanza na kuipita China kwa idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona pamoja na vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo.

Virusi vya corona vimekuwa na matokeo mabaya zaidi kwa Italia kutokana na kuongezeka kwa kasi ya maambukizi kila siku sambamba na vifo.

Hata hivyo, serikali ya Italia imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kujaribu kuzuia kuenea kwa virusi vya corona nchini humo. Moja ya hatua hizo ni kufunga shule na kuzuia watu kutoka majumbani mwao.

Licha ya hatua zilizochukuliwa awali, bado kasi ya maambukizi ya corona iliendelea kuongezeka mara dufu, jambo ambalo liliongeza hofu kwa raia wa nchi hiyo na nchi nyingine ambazo tayari zimethibitisha maambukizi hayo.

Advertisement