Jay Z na Rihanna wachanga dola milioni mbili kusaidia janga la corona

Rapa Jay-Z na mwimbaji Rihanna wameunganisha nguvu na kuchanga dola za Marekani milioni mbili kwa ajili ya kusaidia wenye mahitaji yatokanayo na janga la corona.

Jay Z kupitia mfuko wake wa Shawn Carter, kwa kushirikiana na mfuko wa Rihanna’ wa Clara Lionel, kila mmoja umetoa kiasi cha dola milioni moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wasemaji wa mifuko hiyo, fedha hizo zimetolewa ili kuwasaidia wafanyakazi wasaidizi wa sekta ya afya wanaofanya kazi katika vituo walikohifadhiwa wagonjwa wa corona.

Pia fedha hizo zimetolewa ili kusaidia familia hususani watoto wa wafanyakazi wa sekta ya afya ambao wapo mstari wa mbele kutoa huduma katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa.

“Kiasi cha fedha pia kitawasaidia waliokuwa majumbani ambao hawajiwezi wakiwamo wazee, na waliokuwa na makazi maalumu katika majiji ya New York na Los Angeles.”