Johnson ataka Waingereza wasahau tofauti zao

Muktasari:

Baada ya kushinda uchaguzi kwa kishindo, Waziri Mkuu Boris Johnson ameahidi kuwasikiliza waliopinga mpango wa kujiondoa EU na kwamba ataongoza serikali ambayo ni shirikishi.

London, Uingereza. Waziri Mkuu Boris Johnson amewataka waingereza kusahau miaka ya mgawanyiko uliotokana na mpango wa nchi yao kujiondoa Umoja wa Ulaya (EU) na kuahidi kutumia ushindi wake mkubwa katika uchaguzi kufanikisha azima hiyo ifikapo mwezi ujao.
Alhamisi usiku chama chake cha Conservative kinachotawala Uingereza kilipata matokeo mazuri kuliko yote kilichopata katika miongo mitatu baada ya Johnson kuahidi kufanikisha mpango wa kujiondoa uanachama wa Umoja wa Ulaya ifikapo Januari 31, tarehe mpya ya mwisho iliyowekwa na EY yenye makao yake makuu jijini Brussels.
Uchaguzi huo ulibadilika na kuwa marudio ya kura ya maoni ya mwaka 2016 ya kujiondoa Umoja wa Ulaya, ambayo matokeo yake yalipoozesha viongozi wa Uingereza na kugawanya nchi nzima.
Lakini katika hotuba yake ya ushindi aliyoitoa Downing Street Ijumaa, meya huyo wa zamani wa London alikuwa na sauti ya maridhiano, akiahidi kusikiliza wale waliopinga kujiondoa EU na kuongoza serikali shirikishi.
"Namshauri kila mmoja kutafuta palipoumia na kuruhusu matibabu yaanze," alisema saa chache baada ya kumtembelea Malkia Elizabeth II ili ateuliwe tena kuwa waziri mkuu.
Johnson aliweka rehani hatima yake kisiasa katika uchaguzi huo, ambao uliweka uwezekano wa wanaounga mkono kuendelea kubakia Umoja wa Ulaya kuingia madarakani na kuitisha kura mpya ya maoni ambayo ingeweza kufuta matokeo ya kura ya kwanza.
Lakini kamari aliyocheza ilikuwa na matokeo mazuri baada ya chama chake kushinda viti 365 kati ya 650 vya Bunge-- huo ukiwa ushindi wao mkubwa tangu miaka ya themanini wakati wa Margaret Thatcher.