Kaka wa rais Iran afungwa jela miaka mitano

Muktasari:

  • Awali mahakama iliamkuta na hatia ya kupokea rushwa na ilimuamuru alipe faini na kurudisha fedha alizopewa.

Kaka wa rais wa Iran, Hassan Rouhani ameingia gerezani leo kuanza kutumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya rushwa, shirika la habari la ISNA limeripoti likimkariri mwanasheria wake.
Hossein Fereydoun, ambaye alikuwa akifanya kazi ya msaidizi wa rais, alikamatwa Julai mwaka 2017 na kufikishwa mahakamani mwezi Februari mwaka huu kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za fedha.
Katika uamuzi wa mwisho, hukumu yake ilipunguzwa hadi miaka mitano kutoka saba na ametakiwa kulipa faini pamoja na kutoa fedha alizotuhumiwa kupokea, mahakama ilisema Oktoba mosi.
Mwanasheria wake alisema kaka huyo aliingia gereza la Evin lililopo jijini Tehran leo Jumatano.
"Asubuhi hii, Fereydoun pamoja na mimi tulikuwa katika ofisi ya mwendesha mashtaka," alisema Hossein Sartipi akikaririwa na ISNA.
"Baada ya taratibu za kisheria kumalizika, alichukuliwa kupelekwa gereza la Evin na ameingizwa humo," aliongeza.
Fereydoun alikuwa kama mshauri muhimu na aliyekuwa akitoa nafasi ya kukutana na rais kabla ya kukamatwa.
Ndugu hao wawili hawatumii jina moja kwa sababu Rouhani alibadilisha lake wakati akiwa mdogo na kujiwekea jina linalomaanisha "mtumishi wa Mungu"