Kalonzo adai hamuhitaji tena Raila 2022

Muktasari:

  • Kenya inatarajiwa kuingia katika Uchaguzi Mkuu mwaka mwaka 2022 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuhitimisha miula miwili ya utawala wake

Nairobi, Kenya. Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amesema hahitaji usaidizi wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga ili kushinda kiti cha urais kwenye Uchaguzi Mkuu.

Kenya inatarajiwa kuingia katika Uchaguzi Mkuu mwaka mwaka 2022 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuhitimisha miula miwili ya utawala wake.

Musyoka ambaye katika uchaguzi uliopita aliungana na Odinga Raila na kuwa mgombea mwenza alisema tayari ameanza kujitafutia uungwaji mkono wa Wakenya ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi huo bila kumtegemea kiongozi huyo.

Alisema aliweka kando azma yake ya kuwania urais mara mbili mfululizo ili kumuunga mkono Odinga na kwamba sasa ni wakati wake kutwaa uongozi.

“Huwezi kuomba uongozi. Uongozi hunyakuliwa,” alisisitiza makamu huyo wa Rais wa zamani aliyekuwa akizungumza katika ibada ya mazishi ya baba wa mwakilishi wa wanawake, Joyce Kamene, mzee David Kasimbi.

Viongozi kadha wa eneo la Ukambani ambako ndiko ngome ya Musyoka wanataka makamu huyo wa Rais wa zamani kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu 2022.

 

Katika mikutano kadhaa viongozi hao wamemshinikiza Musyoka kuwa mstari wa mbele katika muungano wowote wa kisiasa utakaoundwa kuelekea uchaguzi mkuu 2022.

Aliyekuwa Seneta wa Machakos, Johnstone Muthama aliwashauri wanasiasa wanaosaka kura za Ukambani kuzungumza na Musyoka kwanza.

Muthama alisema “mkitaka kuongea na sisi ongeeni na Kalonzo kama mmoja wa vigogo wakuu wa kisiasa humu nchini.”

Naye mbunge wa Mavoko, Patrick Makau alisema kuwa Musyoka anatosha kuwa Rais.

“Mwaka 2022 itakuwa kuchagua kati ya nani fisadi na si fisadi. Katikati yetu tuko na mwanamme mweupe kama pamba, anaitwa Stephen Kalonzo Musyoka,” aliambia waombolezaji.