Kamanda Kasingye ataka kesi ya Rais Museveni kumfungia akauti ya Twitter mwanafunzi ifutwe

Muktasari:

Mwanafuzi huyo raia wa Uganda anayeishi nchini Marekani amemshtaki Rais Musevani akishinikiza kiongozi huyo amfungulie akaunti yake ya Twitter.

Kampala, Uganda. Afisa Mkuu wa Siasa wa Polisi Uganda, Asan Kasingye, ameitaka Mahakama Kuu nchini humo kutupilia mbali maombi ya mwanafunzi aliyemshtaki Rais Yoweri Museveni kwa kumzuia katika mtandao wake wa Twitter.

Mwanafunzi huyo anayesoma katika Chuo Kikuu cha Harvard, Hillary Innocent Seguya Taylor, amemfungulia kesi Rais Museveni mahakamani kwa madai kuwa amemzuia kwenye akaunti yake ya Twitter.

Aidha, Rais Museveni ameshtakiwa pamoja na msemaji wa Serikali, Ofwono Opondo na Afisa Mkuu wa Siasa wa Polisi, Asan Kasingye.

Akitoa ushahidi wake leo Jumatatu Novemba 18, afisa huyo wa polisi alieleza mahakama kuwa Rais Museveni anafurahia haki ya kikatiba ya kuamua nani ajiunge na akaunti yake ya kibinafsi.

Alisema Seguya anaweza kupata habari juu ya Uganda au Rais Museveni kupitia mtandao wa jimbo na mashirika tofauti ya vyombo vya habari, kupitia media zao za kijamii na tovuti na si lazima apate kupitia akaunti hiyo.

 Pia, alisema kwamba habari hiyo hiyo inaweza kupatikana kutoka Kituo cha habari kupitia mpango wake rasmi wa Twitter na tovuti yake.

"Nimeshauriwa na mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambako ushauri wao ninaamini kuwa ni kweli kwamba twitter ya  @KagutaMuseveni na @OfwonoOpondo ni za kibinafsi na sio kwa ajili ya ofisi.”

Katika mashtaka aliyowasilisha katika Mahakama Kuu ya Uganda Agosti mwaka huu, mwanafunzi huyo ambaye ni raia wa Uganda anasoma shahada ya uzamivu katika masuala ya uhusiano wa kimataifa, alidai kuwa viongozi hao wamemzuia kupata huduma ya mtandao wa Twitter.

Mwanafunzi huyo amewasilisha madai hayo kupitia kwa wakili wake, Male Mabirizi ambaye atasimamia kesi hiyo kwa kipindi chote ambacho hatokuwapo nchini humo.

Mwanafunzi huyo alidai viongozi hao hutumia akaunti zao za Twitter kama mtandao wa umma kusambaza habari zinazohusiana na mambo ya ofisi hivyo ni lazima wakubali kupata maoni kutoka kwa raia.

Katika mashtaka hayo Seguya anafafanua kuwa, yeye ni raia ambaye anaishi nje ya nchi hivyo ana haki ya kupata habari zinazohusiana na utawala wa nchi yake na kuwasiliana na maafisa husika kupitia vyombo vya habari vya kijamii.

“Kwamba kabla ya kufungiwa, nilitumia jukwaa lile lile la mtandao wa Twiter kuwasilisha maoni yangu, huzuni yangu na mapendekezo kwa maafisa husika.

“Athari ya kunizuia kuingia kwenye akaunti yangu ya Twitter ni kwamba, sasa sina uwezo wa kufuata na kutazama tena mtandao huo na kwa hivyo sina uwezo wa kuwasiliana, kujibu, kupenda, kuweka lebo, kurudisha na kujua habari za umma au kutoa maoni yangu."

Anadai kuwa, Julai 20 akaunti yake ya Twitter yenye jina @HillaryTaylorVI ilifungwa bila kumpa taarifa na Sseguya adai uamuzi wa maafisa hao sio busara kwa sababu akaunti za Twitter zilizotajwa zinatumika kwenye uwanja wa umma kuwasiliana na kupokea maoni kutoka kwa raia na hazijashikiliwa isipokuwa yake tu.