Kemikali ya sumu yaathiri watahiniwa, wasimamizi Kenya

Muktasari:

Walikuwa wanaitumia katika mtihani wa vitendo wa Kemia

Nairobi, Kenya. Idadi kubwa ya watahiniwa wa mitihani ya kidato cha nne na wasimamizi wao wameugua baada ya kuathiriwa na kemikali yenye sumu iliyotumika katika mtihani wao wa Kemia uliofanyika Ijumaa.

Wizara ya Elimu na Baraza la Mitihani la Kenya (Knec) wamenyooshewa kidole kwa kuruhusu kemikali hiyo, xylene inayofahamika kuwa sumu, katika mitihani hiyo wakati inajulikana kuwa inasababisha matatizo ya kiafya na hata kifo.

Katika Jimbo la Trans Nzoia, mwalimu mmoja mjamzito amelazwa katika Hospitali ya Galilee baada ya kupata matatizo yanayohusishwa na kemikali hiyo inayotumika viwandani na katika teknolojia ya tiba.

Mwalimu Cherusha Nyakeri alipelekwa katika hospitali hiyo baada ya kuathiriwa na mvuke uliotokana na kuunguza kemikali hiyo katika Shule ya Sekondari Gidea, iliyopo Kwanza.

Gazeti la The Daily Nation limeripoti kuwa Knec ilielekeza wakuu wa shule wanunue na kutumia kemikali hiyo ikiwa  mbadala wa kemikali nyingine iliyokusudiwa, cyclohexane, ambayo ilikuwa haipatikani sokoni.

Mwanafunzi mmoja katika sekondari ya St Peters Kajulu alilazwa katika Hospitali ya Kombewa Ijumaa baada ya kemikali hiyo kumlipukia usoni na kupata majeraha makubwa ya moto.

Katibu Mtendaji wa Kaunti ya Kisumu, Zablon Awange alisema shule kadhaa, zikiwamo za Kasagam na St Theresa Wasichana zilikumbwa na matukio ya kulipuka kwa kemikali hiyo.

“Tunataka tamko la wizara kuhusu matumizi ya xylene kama kemikali kwenye maabara za Kemia. Xylene ni kemikali yenye sumu inayoweza kusababisha matatizo makubwa kiafya si tu kwa wanafunzi, hata kwa walimu,” alisema.

Aliitaka wizara ya elimu iwalipe fidia wote walioathirika.

“Tumewataka walimu wetu waende kufanyiwa uchunguzi. Hatujui kwanini baraza la Mitani limeamua kutumia xylene kama mbadala wa cyclohexane. Tunataka maelezo,” alisema.

Katika mtihani wa vitendo wanafunzi walitakiwa kuichoma kemikali hiyo na kuangalia moto unaotoka, bila kuwa kizuizi.

Wasimamizi wengi walionusa mvuke huo katika kaunti za Nyeri, Embu na Meru wameripotiwa kuathirika baada ya mtihani.

Mwalimu kutoka Nyeri ambaye hakuitaka kutajwa kutokana na unyeti wa suala hilo, amesema amekuwa mgonjwa tangu Ijumaa na anapata kizunguzungu.

Mtu akivuka mvuke huo kwa kiwango kidogo anaweza kuumua kichwa, kupata kisunguzungu na uchovu lakini akiuvuta kwa wingi  unaweza kuharibu mishipa ya fahamu, kubadilika mapigo ya moyo, kuzimia na hata kifo.

Maofisa wa Baraza la Mitihani hawajatoa taarifa kuhusu tukio hilo.