Kenya kuwabana wakwepa kodi kwa kutumia ukusanyaji mapato kielektroniki

Wednesday November 13 2019Kamishna wa Mkuu wa KRA, James Mburu 

Kamishna wa Mkuu wa KRA, James Mburu  

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Nairobi/Dar. Kenya imepanua wigo wa mradi wa nembo za ushuru za kielektroniki kuyafikia maeneo mengine mapya ya uzalishaji ili kuiwezesha mamlaka kuziingiza biashara nyingi zaidi katika mfumo wa malipo ya kodi kuanzia leo (Jumatano).

Kuanzia leo maji ya kwenye chupa, juisi, vinywaji vya kuongeza nguvu, soda na vinywaji vingine visivyo na vilevi vinavyozalishwa au kuingizwa nchini humo vitakuwa na nembo maalumu ambayo inatolewa na Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) pekee kwa wazalishaji walioidhinishwa.

Kamishna wa Mkuu wa KRA, James Mburu aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter juzi (Jumatatu) kwamba kuanzia leo Jumatano itakuwa mwisho wa uwekaji wa nembo hizo kwenye bidhaa.

“Kwa mujibu wa taarifa yetu ya awali, wazalishaji wote wenye vibali, waingizaji, wasambazaji, wauzaji wa rejareja na umma wote, wanakumbushwa kwamba kuanzia leo Jumatano maji ya chupa, juisi na vinywaji visivyo na vileo vinatakiwa kuwa na nembo maalum ya ushuru,” alisema Mburu.

Kamishna wa Kodi za Ndani KAR, Elizabeth Meyo alisema hivi sasa Kenya ina wazalishaji zaidi ya 130 na waingizaji wa maji ya chupa, juisi, soda, vinywaji vya kuongeza nguvu (Energy drinks) na vinywaji vingine visivyo na vilevi ambao wameshasajiliwa katika mfumo wa kielektroniki wa Utambuzi wa Bidhaa.

“Wauzaji wa rejareja wa maji ya chupa maarufu kama ‘ATM za maji’ wanaweza kupata changamoto kulingana na mazingira ya uendeshaji wa biashara zao, lakini tupo tayari kuwasaidia kikamilifu.

Advertisement

Zaidi ya yote wanapaswa kufahamu kwamba, hatutaruhusu mtu kuendesha biashara nje ya utaratibu kuanzia Novemba 13 kwani tutakuwa hatuwatendei haki wale ambao wametii agizo,” alisema Meyo jijini Nairobi wiki iliyopita.

KRA inatarajia kuingiza biashara nyingi zaidi katika mfumo wa ulipaji kodi ili kukomesha bidhaa zisizo na ubora na kupata mapato takribani bilioni 4 za Kenya baada ya kuimarisha na kuanzisha mfumo huo wa Ulipaji Kodi Kielektroniki (EGMS) ulioanzishwa miaka mitatu iliyopita.

Ulipaji kodi kwa wazalishaji wa maji ya chupa upo katika kiwango cha chini ya asilimia 30 na hivyo mamlaka kupoteza mapato, hali iliyodumu kwa miaka mingi huku viwanda vya uzalishaji maji ya chupa vikivuna mamilioni ya shilingi bila kulipa kodi.

Kwa sasa kuna viwanda 403 vya kuzalisha maji ya chupa vyenye leseni, viwanda vya juisi, soda na vinywaji visivyo na vilevi vipo 42. Hata hivyo, viwanda 64 tu kati ya hivyo ndivyo ambavyo vimesajiliwa katika Mfumo wa Ulipaji Kodi Kielektroniki ambao unaweka nembo iliyounganishwa moja kwa moja na mtandao wa Mamlaka ya Mapato Kenya ili kutoa taarifa ya kiwango cha uzalishaji kila vinapofanya uzalishaji.

Vingine bado havijaingia kwenye mfumo kutokana na kusuasua licha ya muda wa kufungwa kwa zoezi hilo kuahirishwa mara kadhaa ikiwemo Septemba 2019.

Bia, mvinyo, vinywaji vikali na tumbaku vimekuwa vikitumia mfumo huo wa ulipaji kodi tangu KRA ilipoanzisha utaratibu mpya tangu 2015 huku viwanda vingi vikifungwa mara baada ya mfumo huo mpya kuanza.

Kuna viwanda 20 pekee vya vilevi vinavyofanya kazi hivi sasa, idadi ambayo imeshuka kutoka 177 wakati mfumo wa zamani ukiondolewa na kuanzishwa mfumo huu mpya.

Meyo alisema kuwa hakutakuwa na haja ya kupandisha bei ya maji ya chupa na juisi ambavyo ongezeko lake la ushuru ni senti 50 kwa maji na 60 kwa juisi pamoja na gharama za nembo hizo.

Wasimamizi wa KRA wamedai kwamba  wazalishaji wa bidhaa hizo ambao tayari wanatumia nembo hizo wamekuwa wakipandisha bei ya bidhaa kwa siri ili kupata faida kubwa zaidi na kuumiza mlaji.

Kwa kutumia nembo hizi za kielektroniki, KRA sasa itakuwa na uwezo kuzitambua bidhaa ambazo hazijaidhinishwa hata kama tayari zipo sokoni na kuziondoa.

Advertisement