Kimbunga Kimmuri chauwa wawili Filipino

Muktasari:

Watu wawili wamefariki dunia nchini Filipino baada ya kupigwa na Kimbunga Kammuri.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Desemba 4 na kusababisha Kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Manila kufungwa kwa muda baada ya kuharibika vibaya.

Aidha, kimbunga hicho kimesababisha wakazi wa eneo hilo kukosa makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa mapaa kwa upepo mkali.

Kimbunga hicho kiliingia katika pwani ya nchi hiyo kupita eneo la Kusini mwa mji wa Manila wenye watu milioni 13 na kuathiri mashindano ya riadha kwa mataifa ya Asia yanayoendelea katika Jimbo la Kusini Mashariki.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Al Jazeera, mafisa wa hali ya hewa wanaendelea kufanya tathimini za athari za kimbunga hicho.

Kimbunga hicho pia kimesababisha uharibifu mkubwa wa miundominu ikiwamo nguzo za umeme kuanguka.

Taifa la Filipino hukumbwa na wastani wa vimbunga 20 kila mwaka na kusababisha vifo vya mamia ya watu na wengine wakikosa makazi.