Kiongozi wa upinzani Sudan Kusini atishia kujitoa kwenye serikali ya mseto

Muktasari:

  • Serikali ya mseto inayotarajiwa kuundwa mwezi ujao ifikapo Novemba 12 inaweza isifanikiwe kwa sababu kiongozi wa upinzani, Riek Machar amesema hatakuwa sehemu ya serikali hiyo kwa sababu makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana hayajatekelezwa.

Juba, Sudan Kusini. Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar amesema hatakuwa sehemu ya Serikali ya Mseto mwezi ujao kwa sababu makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana hayajatekelezwa.

Machar aliyasema hayo jana Oktoba 20 mjini Juba wakati ametembelewa na ujumbe kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Alisema pande mbili zimeshindwa kukubaliana juu ya kuunganisha jeshi, jambo ambalo ni muhimu zaidi katika mkataba wa amani uliosainiwa mwaka jana na haoni kama wanaweza kuunda serikali bila jambo hilo.

“Sisi SPLM-IO hatutakuwepo kwa sababu hatutaki kuiweka nchi kwenye matatizo. Kitu kilichokuwa kinahitajika ili kuunda serikali hakipo,” alisema Machar kama alivyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Rais Salva Kiir na Machar walisaini mkataba wa amani Septemba 2018 baada ya mfululizo wa makubaliano kuvunjika na kusababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamesababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu na wengine kuyakimbia makazi yao.

Hata hivyo, ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulisema tatizo lililobainishwa na Machar linaweza kutatuliwa kabla ya Novemba 12 ambapo pande hizo mbili zitasaini makubaliano na kuunda serikali ya pamoja.

“Kitu anachokisema Machar kinaweza kufanyika ndani ya wiki tatu zijazo lakini kinahitaji viongozi wa kisiasa kusema tunakwenda kufanya hilo,” Balozi wa Afrika Kusini, Umoja wa Mataifa (UN), Jerry Matjila aliwaeleza waandishi wa habari.

Balozi wa Marekani – UN, Kelly Craft alisema bado wanaitambua Novemba 12 kama siku ya ukomo wa kufikiwa kwa makubaliano ya amani baina ya pande hizo mbili.

“Tunatarajia serikali na wapinzani kuungana pamoja na kuwa tayari kuwaweka watu wao mbele,” alisema Balozi Craft.

Mei mwaka huu, pande mbili zilikubaliana kuanzisha serikali ya pamoja ndani ya miezi sita na Septemba walisema wataunda serikali ya mpito kufikia Novemba 12 kama sehemu ya makubaliano hayo.

Makubaliano hayo hayakufikiwa kwa sababu serikali ilisema haina fedha za kupunguza silaha na kuunganisha jeshi la nchi hiyo na vikosi vya upinzani.