Korti yabariki Zuma kupandishwa kizimbani

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma sasa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya rushwa baada ya mahakama kutupilia mbali ombi lake la kutaka kesi hiyo isitishwe kabisa.

Uamuzi huo wa leo una maana kuwa kutakuwa na uchunguzi zaidi kuhusu mpango wa ununuzi wa silaha wa mwaka wa 1999 ambao Zuma anatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni ya kutengeneza silaha ya Ufaransa, Thales.

Tuhuma hizo ziliibuliwa miaka kumi iliyopita lakini zikaondolewa, na kurejeshwa tena baada ya Ofisi ya Mashtaka kutangaza kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kumfikisha kizimbani.

Zuma alikuwa rais kutoka mwaka wa 2009 hadi 2018, wakati alipolazimishwa kujiuzulu na chama tawala cha ANC kutokana na madai mengine tofauti ya rushwa.

Hata hivyo, Zuma anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.